Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha ushirika Mapendo kilichopo Kijiji cha Mpepo Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Hyasint Whero kushotoa,akiwaongoza baadhi ya wakulima wa kahawa kuondoa majani yasiyohitajika kwenye shamba la kahawa ili kupata kahawa bora(Picha na Muhidin Amri).
Katibu wa Chama cha msingi cha ushirika Mapendo Amcos kata ya Mpepo Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma Pankras Komba kulia,akiwaonyesha baadhi ya wakulima wa kahawa wanaohudumiwa na Chama hicho sehemu ya kuanika kahawa kabla ya kufikishwa kwenye maghala kwa ajili ya kuuzwa(Picha na Muhidin Amri)
Na Muhidin Amri,Nyasa
WAKULIMA wa zao la kahawa katika kijiji cha Mpepo Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mbolea za ruzuku ambayo imesaidia kuleta tija na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Wamesema,mbolea ya ruzuku imepunguza gharama za uzalishaji na kuwezesha kuajiri nguvu kazi zaidi kwenye mashamba yao ikilinganisha na miaka iliyopita kabla ya Serikali kuanza kutoa mbolea ya ruzuku kwenye zao la kahawa.
Ilbert Mahai mkulima wa kijiji cha Mpepo alisema,baada ya kupata mbolea ya ruzuku,amepunguza gharama na fedha alizokuwa akitumia kununua pembejeo kwa ajili ya shamba lake lenye ukubwa wa ekari 19 na sasa gharama hizo amezielekeza kulipa vibarua, hivyo kuwa sehemu ya ajira kwa wananchi wengi wa kijiji hicho na vijiji vingine hasa vijana na wanawake.
Alisema,tangu alipoanza kupata mbolea za ruzuku uzalishaji umeongeza kutoka tani 20 msimu wa kilimo 2022/2023 hadi tani 90 msimu wa mwaka 2023/2024 na msimu wa kilimo 2024/2025 amezalisha zaidi ya tani 150.
Alisema,katika msimu wa kilimo 2025/2026 anategemea uzalishaji utaongezeka hadi tani 200 hasa baada ya Chama cha msingi cha ushirika Mapendo kuwahisha mbegu na pembejeo ambazo zimewezesha kufanya maandalizi ya kilimo cha zao hilo mapema.
Mahai amewataka wananchi wenzake wa Nyasa hususani vijana,kujikita zaidi kwenye kilimo cha zao la Kahawa kwani lina faida kubwa kiuchumi kutokana na kuongezeka kwa bei kutoka Sh.4500 msimu 2023 hadi Sh.10,000 msimu 2024/2025 kwa kilo moja.
Ameishauri Serikali kuhakikisha inapeleka pembejeo kwa wakati ili wakulima waanze maandalizi mapema hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji na kupata kahawa bora inayokubalika kwenye soko la ndani na nje ya nchi.
Alto Matembo mkulima wa kijiji cha Ndondo alisema,anapenda kulima zao la kahawa kwani amepata manufaa makubwa ikiwemo kujenga nyumba bora,kusomesha watoto kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu.
Matembo,amewashauri vijana wa kijiji hicho kujikita kwenye kilimo cha zao la kahawa, kwa sababu lina manufaa makubwa kiuchumi na kujiunga kwenye vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) vyenye jukumu la kukusanya kahawa na kuzipeleka sokoni ili kupata soko la uhakika.
Ameiomba Serikali kupitia wizara ya kilimo, kuendelea kutoa pembejeo za ruzuku kila mwaka na kusimamia bei ya pembejeo ili kuwapunguzia gharama ya kusafiri kwenda Wilaya jirani ya Mbinga umbali wa kilometa 98 kufuata pembejeo ambazo gharama ya kusafirisha mfuko mmoja wa kilo 50 ni Sh.5,000 hadi 6,000.
Mkulima mwingine wa kijiji cha Mtetema kata ya Mpepo Method Ngonyani,ameishukuru Serikali kuanzisha mradi wa kuzalisha miche bora ya kahawa aina ya Kombat ambao umesaidia wakulima kupata miche bora na kwa urahisi zaidi.
Alisema,miche hiyo inayozalisha katika kijiji chao imehamasisha wakulima ambao awali walijikita kwenye mazao mengine kama mahindi na maharage ambayo hayana faida kubwa ikilinganisha na zao la kahawa.
Alisema,kupitia mradi huo sasa hawapati usumbufu wa kwenda Wilaya ya Mbinga kununua miche ya kahawa kwa bei ya juu badala yake miche inatolewa bure na Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya Nyasa na Bodi ya Kahawa Tanzania(TCB).
Ameiomba Serikali kupitia bodi ya kahawa Tanzania kuongeza uzalishaji wa miche ya kahawa kwani mahitaji ni makubwa kutokana na watu wengi kuhamasika kwenye kilimo cha zao hilo.
Katibu wa Chama cha Msingi cha Ushirika Mapendo Amcos Panglas Komba alisema,ili kuwapunguzia wakulima gharama ya kusafirisha kahawa kwenda maeneo mengine ili kusindika kahawa, Chama hicho kimenunua mtambo wa kuchakata kahawa wenye uwezo wa kuhudumia wakulima 200 kwa wakati mmoja.
Alisema,katika msimu wa kilimo 2024/2025 wamefanikiwa kuchakata tani zaidi ya 50 zilizoletwa na wakulima 126 kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nyasa.
Mapunda alisema,licha ya mafaniko hayo lakini changamoto kubwa ni uwezo mdogo wa mtambo huo,kwani uwezo wake ni kuchakata kilo 5,000 za kahawa mbichi wakati mahitaji ya wakulima ni makubwa.
Ameiomba Serikali kupitia Wizara ya kilimo, kuwapatia mashine yenye uwezo mkubwa ili kurahisisha kazi ya uchakataji ili wakulima waweze kuwahi soko na bei nzuri kupitia minada ya kahawa inayofanyika.
Alisema,kabla ya kupata mtambo huo wakulima walikuwa wanavundika na kusindika kahawa majumbani,hata hivyo changamoto kubwa ilikuwa kupungua kwa ubora kwa sababu maandalizi hayakuzingatia taratibu na kanuni bora za usindikaji wa kahawa.
Amewashauri wakulima,kuacha kuchakata kahawa majumbani kwa kuwa inapunguza ubora,badala yake watumie mtambo wa Chama chao kusindika kahawa ili kupata kahawa bora,yenye radha na bei nzuri.