Mhifadhi na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mbinga Mheshimiwa Ngwatura Ndunguru akielezea historia ya Jemedari wa kabila la Wamatengo Kayuni Makita wa kwanza aliyeuawa kwa kukatwa kichwa na askari wa kukodi wa waarabu wakati wa vita ya makabila kati ya wangoni na wamatengo mwaka 1885 ambaye alizikwa katika kijiji cha Mbuji.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la wazee wa Mila wa Kabila la wamatengo wakiwa katika picha ya pamoja katika kaburi la Jemedari wao Makita wa kwanza katika kijiji cha Mbuji Mbinga.
……….
Na Albano Midelo.
Katika kijiji cha Mbuji kilichojificha kwenye vilima vya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kuna kaburi la aina yake kaburi linalobeba historia ya maumivu, ujasiri, usaliti, na ushindi. Hili si kaburi la kawaida.
Ni kaburi la Jemedari wa vita, Mtawala wa kwanza wa kabila la Wamatengo, Chifu Kayuni Kapitangana Ndunguru Makita, ambaye si tu alipigana vita vya ukombozi dhidi ya Wangoni, bali pia aliuawa kikatili na kisha kuzikwa akiwa amekalishwa katika kaburi la mviringo kama ishara ya heshima kuu kwa mashujaa waliotangulia.
Hii ni hadithi ambayo haijasimuliwa sana, lakini inayobeba uzito mkubwa wa historia ya makabila ya Kusini mwa Tanzania hadithi ya kiongozi aliyekuwa zaidi ya mtawala; alikuwa ngao ya taifa lake.MIAKA YA MOTO NA MAPAMBANOIlianza mwaka 1824 hadi 1885.
Chifu Makita akiwa kijana mwenye ujasiri na hekima ya ajabu, alitokea kuwa kiongozi wa mapambano makali kati ya Wamatengo na Wangoni – kabila lililovamia kutoka Kusini mwa Afrika na kujaribu kutwaa maeneo ya Kusini mwa Tanzania.
Makita hakusita,alikusanya vijana mashujaa, akawatayarisha, na kuwaongoza kwenye vita vikali vilivyodumu kwa miaka mingi.Kwa mujibu wa Mheshimiwa Ngwatura Ndunguru Afisa Wanyamapori Mstaafu na Mbunge Mstaafu wa Mbinga,Chifu Makita alikuwa siyo tu kiongozi wa kijeshi, bali pia mfanyabiashara mwenye ushawishi mkubwa.
Kipaji chake cha kipekee cha kuongoza kilimfanya kuwa tishio kwa maadui na tegemeo kwa jamii yake.”Alikuwa Amiri Jeshi Mkuu wa vita. Hakuanza kama chifu, bali mashujaa waliomzunguka walimtambua kwa uwezo wake wa kipekee wa kuongoza na kushinda vita,” anasema Ndunguru.
USALITI NA KIFO CHA KISHUJAABaada ya ushindi mkubwa dhidi ya Wangoni katika eneo la Litembo, Makita alionekana kuwa tishio hata kwa washirika wake wa kibiashara.
Waarabu waliokuwa wakishirikiana na baadhi ya makundi ya Kingoni. Katika kile kilichoaminika kuwa mpango wa usaliti, mwarabu mmoja ambaye alikuwa askari wa kukodi alikata kichwa cha Makita kwa ghafla, kwa hila na tamaa ya mamlaka.
Hicho kichwa kilichokatwa kilikimbizwa mbali na maadui kama ishara ya udhalilishaji wa kiongozi mkubwa wa Wamatengo. Lakini historia haikuishia hapo.
SHUJAA MWANAMKE NA UKOMBOZI WA KICHWAKatika simulizi inayoshangaza na kuamsha hisia za uzalendo, mama mmoja jasiri kutoka jamii ya Wamatengo alijitokeza.
Alijulikana kwa jina la Kingengi mwanamke aliyekuwa akiaminika kuwa na uwezo wa kiroho usio wa kawaida. Kwa ujanja na ujasiri, aliwafuata wale waliokuwa na kichwa cha Chifu Makita.
Akiwa amejificha nyuma ya vicheko na michezo ya kitamaduni, alifanikiwa kuiba kichwa hicho kutoka kwa maadui waliokuwa wamelewa usingizi.Usiku huo huo, wazee wa kijiji walikusanyika. Kwa heshima ya shujaa wao, walikiunganisha kichwa na kiwiliwili cha Makita, wakamkalisha kama ilivyo desturi ya maziko ya heshima ya juu, na kumzika kwa siri kubwa kijijini Mbuji.
Na si hilo tu vijana sita waaminifu, mashujaa waaminifu waliompenda Chifu wao, walizikwa hai pamoja naye kama ilivyoaminika kwamba mtu mkubwa hawezi kuzikwa peke yake bila watu wa kumhudumia “ng’ambo ya pili”.
URITHI ULIOFICHIKA, URITHI UNAOSUBIRI KUSIMULIWALeo, miaka zaidi ya 140 baadaye, kaburi hilo limesimama Mawe yaliyotumika kujenga kaburi hilo, kwa mujibu wa Ndunguru, yalipangwa kwa heshima maalum, kwa kushirikisha familia na viongozi wa kijiji, mwaka 2004 alipokuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga.
“Historia ya Wamatengo bado haijaandikwa vizuri.
Serikali inapaswa kushirikiana na baraza la mila la wamatengo kuhakikisha simulizi hizi hazipotei. Maeneo kama haya yana thamani kubwa ya kihistoria na utalii wa kiutamaduni,” anashauri Ndunguru.
Hadithi ya Chifu Makita si ya huzuni tu, bali ni mwito wa kuamka. Ni sauti ya historia inayoibuka kutoka kaburini ikitaka kusimuliwa.
Katika enzi ya sasa ambapo mataifa mengi yanainua hadhi ya mashujaa wao wa kale, Mbinga nayo inayo hadithi ya kutisha na ya kishujaa hadithi ya mtu aliyezikwa akiwa ameketi, huku vijana sita wakijitolea maisha yao kumsindikiza.Ni wakati wa Serikali, wanahistoria, na wazalendo kuifukua historia hii.
Kwa sababu kama kuna kiongozi ambaye anastahili heshima ya kitaifa kwa ujasiri na mapambano ya kulinda mila na ardhi ya wazawa, basi huyo si mwingine bali ni Chifu Makita shujaa asiyeweza kufutika katika kumbukumbu za Ruvuma, Tanzania, na Afrika nzima.