Watu ishirini na nane (28) wamefariki dunia na wengine tisa (9) kujeruhiwa katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha magari matatu katika eneo la Mlima Iwambi, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, mkoani Mbeya.
Akizungumza kuhusu ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Benjamin Kuzaga, amesema kuwa tukio hilo limetokea mnamo tarehe 07 Juni 2025, majira ya saa 1:47 usiku, katika barabara kuu ya Mbeya – Tunduma.
Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Scania lenye namba za usajili T.830 EDP na tela namba T.148 CTD, mali ya Hussein Hilal Malick, likiendeshwa na dereva Philipo Laiton Mwashibanda (33), mkazi wa Tunduma, ambaye alikuwa akitokea Dar es Salaam kuelekea Zambia akiwa na shehena ya unga. Gari hilo lilishindwa kudhibitiwa na kugonga kwa nyuma magari mawili:
Gari namba T.257 DVP, aina ya Mitsubishi Rosa, lililokuwa limebeba abiria. Gari namba T.185 DMF, aina ya Toyota Lite Ace.
Baada ya kugonga magari hayo, lori hilo lilitumbukia kwenye bonde la Mto Mbalizi na kusimama kwenye gema/ukingo wa mto, hali iliyosababisha vifo vya watu 28.
Majina na Takwimu za Waliopoteza Maisha Kati ya watu waliofariki: Wanawake: 12 (wakiwemo watoto 2)
Wanaume: 16 (wakiwemo watoto 2)
Hadi sasa, miili 18 imetambuliwa na ndugu wa marehemu, wakati miili 9 bado haijatambuliwa.
Majeruhi
Watu 9 walijeruhiwa, kati yao: Wanaume: 7, Wanawake: 2, Majeruhi waliotajwa kwa majina ni:
Baraka Samuel Mgala (35), mkazi wa Mbalizi, aliyekuwa dereva wa Mitsubishi Rosa – ameumia miguu yote miwili, mbavu na kichwani.
Philipo Laiton Mwashibanda (33), dereva wa lori aina ya Scania – amevunjika mguu wa kushoto.
Chanzo cha Ajali
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa lori, ambaye alishindwa kulimudu gari katika eneo la mteremko mkali wa Mlima Iwambi.
Mtuhumiwa huyo kwa sasa anashikiliwa na Polisi akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Ifisi chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali hiyo hiyo, na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu.
Wito wa Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu na majeruhi wa ajali hii. Aidha, linatoa wito kwa madereva wote kuwa waangalifu, kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuchukua tahadhari katika maeneo hatarishi ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.