Na.Meleka Kulwa_DODOMA
Akifungua rasmi kambi maalum ya elimu, uchunguzi wa afya, na matibabu, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti, na Ushauri wa UDOM, Prof. Razack Lokina, alisema kuwa lengo kuu la kongamano hilo ni kuonyesha ushahidi wa tafiti na kutoa ufumbuzi wa changamoto za kiafya.
“Kambi hii maalum inayofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 10 Juni 2025 inatarajiwa kuhudumia wananchi wasiopungua 1,500 kwa siku,” alisema Prof. Lokina.
Kongamano hilo litakaloanza rasmi tarehe 11 hadi 13 Juni 2025 litahusisha zaidi ya watu 500 kutoka ndani na nje ya nchi, huku mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Hombolo, Dkt. Emmanuel Kitumba, ameishukuru serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya bora katika kituo hicho. “Kwa sasa huduma zote muhimu zinapatikana hapa kituoni, ikiwa ni pamoja na dawa ambazo sasa zinapatikana kwa asilimia kubwa,” alisema Dkt.Emmanuel Kitumba.
Aliongeza kuwa wananchi wa Hombolo wananufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na kambi hio ya afya inayoendelea, ambapo huduma zote zinatolewa bila malipo.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dkt. Alfred Meremo, alisema kuwa lengo kuu la kambi hio ni kutoa huduma bora kwa jamii na kuchangia ufumbuzi wa changamoto za kiafya. “Jukwaa hili limewaleta pamoja watafiti, wataalamu wa afya, na wahadhiri ili kuhimiza uchunguzi wa afya mapema na kuelimisha umuhimu wa mazoezi.
Pia, tunatoa huduma maalumu kama upandikizaji wa uloto na figo kwa mara ya kwanza kwa ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara,” alisema Dkt. Meremo. Aliongeza kuwa kongamano hilo litahusisha wananchi zaidi ya 1,500 kwa siku mbili
Amidi wa Shule Kuu ya Tiba na Afya ya Kinywa UDOM, Dkt. Shakilu Jumanne, aliwahimiza wananchi wa Hombolo kufika kituoni kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, yanayoambukizwa na yasiyoambukizwa, huku wakipata elimu ya kujikinga na magonjwa hayo.
“Kupitia kongamano hili, tunafanya uchunguzi na kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali za kiafya kwa kushirikiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa,” alifafanua.
Mhadhiri wa UDOM, Leonard Kitalambula, alieleza kuwa sababu ya kufanyika kwa kambi hio katika Kituo cha Afya Hombolo ni kutokana na wingi wa wananchi katika eneo hilo. “Tumepitia maeneo tofauti ndani ya Dodoma, na kwa sasa tuko Hombolo baada ya kuwa Chamwino awali,” alisema.
Wananchi wa Hombolo wameonyesha furaha na shukrani kwa kongamano hilo. George Karebi, mkazi wa kijiji cha Hombolo, alisema kuwa huduma zinazotolewa zimekuwa msaada mkubwa kwake. Naye Bi. Mwajuma Ramadhan alilishukuru Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuwapatia matibabu bora bila malipo ambayo wangelazimika kulipia sehemu nyingine.
Kwa ushirikiano wa wataalamu wa afya wa UDOM na Hospitali ya Benjamin Mkapa, kongamano hilo linaonyesha dira ya kuboresha huduma za afya na maisha ya jamii kwa ujumla.