Wakurugenzi wa Halmashauri zote sita za Mkoa wa Njombe wametakiwa kusimamia kwa ukaribu mashine 20 za kuongeza virutubisho kwenye unga wa mahindi ili kuweza kusaidia katika mapambano dhidi ya udumavu mkoani humo.
Agizo hili limetolewa juzi na Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Judica Omari, wakati akikabidhi mashine hizo zilizotolewa na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF).
Alisema mashine hizo zitatumika kuongeza virutubisho katika unga wa mahindi, kitu ambacho kinatarajiwa kuboresha afya za watoto na kupunguza tatizo la udumavu katika jamii.
Kwa upande wake, Ofisa Lishe wa Mkoa wa Njombe, Betha Nyigu, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa viashiria vya mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024, alieleza mafanikio yaliyopatikana ambapo wamefanikiwa kupunguza kiwango cha udumavu kutoka asilimia 50.2 hadi 40.2.
Naye, Prof. Lilian Pasate kutoka Taasisi ya Chuo Kikuu cha Nelson Mandela alielezea umuhimu wa ubunifu wa uji wa chap chap, ambao unachangia katika kupunguza tatizo la udumavu kutokana na urahisi wa uandaaji wake.
Katika kuimarisha hali ya lishe mkoani Njombe, viongozi na wananchi wametakiwa kujitathmini kuhusu ushiriki wao katika kutekeleza Mkataba wa Lishe. Ufuatiliaji na tathmini vimetajwa kuwa nyenzo muhimu katika kubaini changamoto na kuboresha afua za lishe katika jamii.