Akizungumza leo, Juni 9, 2025, jijini Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Siku ya Chakula Salama Duniani, Mhe. Kigahe amesema kuwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa Mpango huo wa Kitaifa kwa lengo la kulinda afya ya wananchi na kuimarisha mifumo ya chakula nchini.
Mhe. Kigahe amesisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kwenda kinyume na taratibu za usalama wa chakula.
“Kupitia mpango huu, tunalenga kuimarisha afya za wananchi. Changamoto kubwa tuliyonayo siyo upatikanaji wa chakula, bali ni kuhakikisha chakula hicho ni salama kwa matumizi ya binadamu,” amesema Mhe. Kigahe.
Ameongeza kuwa hatua ya kwanza ni kuhakikisha usalama wa chakula ni uzalishaji wa kutosha, jambo ambalo Serikali imefanikiwa kwa kiwango kikubwa, na sasa jukumu lililopo ni kuhakikisha chakula hicho kinakuwa salama.
Mhe. Kigahe amebainisha kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara, kupitia TBS, ina jukumu la kusimamia ubora wa bidhaa zote, na hivyo imeadhimisha siku hiyo kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu wajibu wa kila mmoja katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula salama.
“TBS imeweka mpango mzuri wa kusaidia wazalishaji kuzingatia viwango vya ubora, ili kuhakikisha wananchi wanapata chakula bora na salama,” amesema Mhe. Kigahe.
Aidha, Naibu Waziri amezielekeza halmashauri zote nchini kushirikiana na taasisi za sekta mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chakula salama.
Amewataka wananchi kuwa waangalifu kwa kusoma lebo za bidhaa, kuchunguza ubora wa chakula na kuzingatia usafi katika maandalizi na uuzaji wa vyakula.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Profesa Othman Chande, amesema TBS itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha kuwa kila chakula kinachouzwa sokoni kinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
Profesa Chande amesisitiza kuwa usalama wa chakula ni msingi wa afya ya taifa na maendeleo ya kiuchumi, huku akieleza Shirika hilo limekuwa likichukua hatua madhubuti kuhakikisha kila mwananchi anapata chakula chenye viwango vinavyokubalika kwa usalama wa mlaji.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema kuwa athari za chakula kisicho salama ni pamoja na kushuka kwa nguvu kazi ya taifa kutokana na magonjwa yanayotokana na matumizi ya vyakula visivyo salama.
Amesema kuwa TBS kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa Mpango wa Kitaifa wa kukabiliana na dharura za chakula hatarishi, ambao utasaidia kuchukua hatua za haraka na kinga endapo litatokea tatizo la usalama wa chakula nchini.
“Tunatoa wito kwa jamii kuzingatia sayansi katika hatua zote za maandalizi ya chakula, kwa sababu athari za chakula kisicho salama zinaweza kusababisha magonjwa na hata vifo,” amesema Dkt. Katunzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wanachama kutoka Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Bi. Neema Mhondo, amesema viwanda vina nafasi muhimu katika kuhakikisha uzalishaji na usambazaji wa chakula salama chenye ubora na viwango vinavyotakiwa.
“Kwa kushirikiana na TBS na wadau wengine wa kimataifa, tunaendelea kujenga uwezo wa kufanikisha viwango vya kimataifa vya usalama wa chakula. Tunawashukuru TBS kwa ushirikiano wao wa karibu katika kufanikisha agenda hii muhimu,” amesema Bi. Mhondo.
Maadhimisho ya Siku ya Chakula Salama Duniani kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu: “Chakula Salama, Sayansi kwa Vitendo.”
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe akizindua Mpango wa Kitaifa wa kukabiliana na dharura zitokanazo na chakula kisicho salama katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Salama Duniani iliyofanyika leo Juni 9, 2025 jijini Dar es Salaam

