Dar es Salaam, 09 Juni 2025,
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imesaini makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitatu na Aspire Educational Technologies kutoka United Arab Emirates, kwa lengo la kukuza elimu kupitia uandaaji wa maudhui ya kidijitali kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini.
Hafla ya utiaji saini imefanyika katika makao makuu ya ofisi za TET jijini Dar es Salaam. Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba, alisema kuwa tukio hilo linaashiria mwanzo wa ushirikiano wa kimkakati kati ya pande hizo mbili na limekuja kwa wakati muafaka ambapo Serikali imeanza kutekeleza mtaala ulioboreshwa.
“Hii kwetu imekuja wakati mzuri kwani kwa sasa mtaala ulioboreshwa unasisitiza kukuza stadi za Karne ya 21 kwa wahitimu zikiwemo ubunifu, kutatua matatizo, uzalendo, fikra tunduizi, ushirikiano na ujuzi wa kidijitali. Makubaliano haya yamelenga kujenga stadi hizi, hususan stadi ya ujuzi wa kidijitali,” alisema Dkt. Komba.
Kupitia makubaliano hayo, Aspire itahusika katika kuandaa maudhui ya elimu ya kidijitali yenye ubora wa hali ya juu, yanayoendana na mtaala wa Tanzania, huku TET ikihakikisha kuwa maudhui hayo yanaidhinishwa kwa kuzingatia miongozo na viwango vya elimu vya kitaifa.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Aspire Educational Technologies, Bw. Rahul D’Mello, alieleza kufurahishwa na ushirikiano huo, akisema kuwa ni fursa adhimu kwa taasisi yake kushiriki katika kuboresha elimu kwa njia za kidijitali nchini Tanzania.
“Ni jambo kubwa kwetu kupata nafasi ya kuweza kufanya kazi na TET katika eneo la kuwezesha uandaaji wa maudhui kwa njia ya kidijitali kwa lengo la kusaidia wanafunzi,” alisema Bw. D’Mello.
Makubaliano haya yanatarajiwa kuleta mageuzi chanya katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanaimarishwa katika ufundishaji na ujifunzaji, kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi sekondari.