BABA mzazi wa marehemu Beatrice Magombola, Deograce Magombola huku akibubujikwa na machozi, ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa polisi walimwambia mtoto wake (Beatrice) ameuliwa na mama yake mzazi pamoja na mdogo wake.
Magombola ambaye ni shahidi namba 13 katika kesi ya mauaji ya kukusudia inayomakabili mtoto wake Alphonce Magombola na mtalaka wake Sophia Mwenda amedai hayo Juni 9,2025 mahakamani hapo.
Akiongozwa na wakili wa serikali Violeth David kutoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mary Mrio, aliyepewa mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi hiyo, Magombola amedai mwaka 2022 alipokea taarifa za kifo cha Beatrice kutoka kituo cha polisi Oysterbay jijini Dar Es Salaam na kwamba kipindi hicho, Beatrice alikuwa amemchukua Sophia kuishi nae (Mama yake mzazi) pamoja na mtoto wake.
Akiendelea kutoa ushahidi wake, wakili Violeth alimuonesha picha Magombola na kumuhoji kama anamfahmu mtu aliyekuwa katika picha hizo…ndipo Magomboa alishika na kuziangalia kisha alianza kutokwa na machozi huku akimuonesha picha hizo hakimu na kusema kuwa “huyu ni mwanangu , Beatrice’ kisha akazibusu picha zile akiendelea kutokwa machozi kwa muda.
Magombola amedai, Desemba Mosi, 2020 asubuhi, ilikuwa mara yake ya mwisho kuwasiliana na mtoto wake Beatrice ambaye walizungumza kuhusu kesi aliyoifungua mahakamani kutokana na Sophia kuuza nyumba ya familia iliyopo Mbeya na kwamba Beatrice alitakiwa kwenda kutoa ushahidi Desemba 7, 2020.
Akielezea zaidi Magombola ambaye ni Mhadhiri Mstaafu chuo cha Tengelu Arusha amedai mwaka 1986 alifunga ndoa na Sophia (mshtakiwa) na walibahatika kupata watoto wanne ambao ni Beatrice (marehemu) Alphonce (mshtakiw), Rechal na Deslius, Mwila na walitalikiana mwaka 2008.
Shahidi huyo aliendele kudai kuwa katika watoto wake hao, Beatrice kwasasa ni marehemu, Alphonce ni mtuhumiwa katika kesi hiyo ya mauaji, Rachael anaishi Zanzibar na Mwila anaishi Arusha.
Amedai kabla ya kupata taarifa za kifo cha Beatrice alijaribu kumtafuta kwa njia ya simu ya mafanikio.
“Nilimtafuta Desemba 2, sikumpata hewani, niliendelea kumtafuta bila mafanikio, nilizani mama yake (Sophia), amemzuia asije kutoa ushahidi, niliendelea kumtafuta kazini kwake Ofisi za Tasaf wakanambia ameshamaliza mkataba, nilimtuma mtoto wa kaka yangu anaitwa Mariam akamwangalie katika makazi yake Kijichi, akaambiwa ameshahama, nilimpigia Sophia hakuwa hewani” amedai Magombola.
Ameendelea kudai kuwa, mwaka 2022,alipigiwa simu na mtoto wa kaka yake anayeitwa Alice na kumweleza kuwa ameona katika mitandao ya kijamii kwamba Alphonce (mtoto wake) anachangisha fedha kwa marafiki wa Beatrice waliosoma wote Uganda, wamchangie kwasababu anaumwa sana na amelazwa hospitalini Afrika Kusini, taarifa ambazo hakuwa nazo.
Amedai, baada ya muda akiwa nyumbani kwake Arusha alipigiwa simu na polisi kutoka kituo cha Oysterbay na kumweleza kuwa Beatrice ameuwawa na walitaka afike Dar es Salaam akatoe maelezo kuhusu anachokifamamu.
“Nilikuja Dar es Salaam, polisi waliniambia Sophia na Alphonce ndio waliomuua Beatrice, walinichukua sampuli kwangu kwa ajili ya kipimo cha vinasaba, pia tulienda kufukua mwili wa Beatrice katika makabuli ya Bagamoyo eneo la Ukuni, tulipofika na kuoneshwa kaburi mimi sikuweza kustahimili, niliishiwa nguvu ,nikarudishwa nyumbani kutibiwa” alidai Magombola.
Alidai, baada ya taratibu za polisi kukamilika , Novemba 2023, waliomba kibali cha mahakama kuruhusu kuzika mwili wa Beatrice kijijini kwao Masimbwe, Igelango wilaya ya Njombe na waliruhusiwa.
Kesi itaendelea kesho.