Missenyi, Kagera.
Na Silivia Amandius.
Wafugaji katika Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera wameeleza kuridhishwa kwao na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, wakisema imeleta mageuzi chanya katika sekta ya ufugaji ambayo kwa muda mrefu haikupata msukumo wa kutosha.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wa wilaya hiyo katika mahojiano na waandishi wa habari yaliyofanyika kata ya Mutukula, Mwenyekiti wa Wafugaji wa Missenyi, Abdul Majid Kayondo, alisema kuwa maendeleo yanayoonekana sasa ni ya kihistoria na yanatoa matumaini mapya kwa wafugaji.
“Kwa kweli tumeshuhudia mabadiliko makubwa ambayo yameleta manufaa makubwa kwetu. Serikali imetufikia kwa ukaribu zaidi, tumepatiwa elimu ya kisasa ya kilimo na ufugaji, jambo ambalo halikuwepo miaka ya nyuma,” alisema Kayondo.
Kayondo alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wafugaji umeimarika sana, akieleza kuwa sasa viongozi wa juu wa wizara husika wapo karibu na wananchi na wanajibu mahitaji yao kwa haraka.
“Kipindi cha nyuma ilikuwa vigumu mno kumuona au kuzungumza na waziri mwenye dhamana, lakini sasa tunashauriana nao na wanatufikia kwa haraka pindi tunapowahitaji,” aliongeza.
Aidha, aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika kilimo na ufugaji, badala ya kung’ang’ania ajira rasmi ambazo ni chache, akisisitiza kuwa sekta hizo zina uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yao.
Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Wilaya ya Missenyi, Dkt. Edward Aligawesa, alisema kuwa sekta ya ufugaji imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa halmashauri hiyo, akiwataka wafugaji kuendelea kutumia minada na rasilimali zilizopo kwa tija zaidi.
Aliongeza kuwa uzalendo na uwajibikaji wa wafugaji ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu, huku akiwahimiza kuwa wabunifu na kushirikiana na Serikali katika kuboresha maisha yao na kuchangia pato la taifa.
Mwenyekiti Kayondo alihitimisha kwa kuahidi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha vijana wanapata maarifa sahihi ya kisasa katika ufugaji na kuwa chachu ya maendeleo katika wilaya ya Missenyi na Mkoa wa Kagera kwa ujumla.