Dar es Salaam, 05 Juni 2025 – Benki ya CRDB imeandika ukurasa mpya wa mafanikio baada ya kutangazwa mshindi wa tuzo ya Benki Bora kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SME) katika hafla ya tuzo za sekta ya benki barani Afrika ‘African Banker Awards 2025,’ iliyofanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) jijini Abidjan, Côte d’Ivoire.
Kaulimbiu ya mwaka huu wa tuzo hizo ilikuwa “Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo Endelevu,” ikiakisi umuhimu wa sekta ya fedha katika kuchochea ukuaji wa kijani, ujumuishi wa kijinsia na uhimilivu wa kiuchumi barani Afrika.
Katika mwaka huu ambapo Benki ya CRDB inaadhimisha miaka 30 ya huduma ubunifu, ilipata heshima ya kutajwa katika vipengele vinne vikuu, vikiwemo: Benki Bora kwa Wajasiriamali (Mshindi), Banker of the Year – kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki, Abdulmajid Mussa Nsekela, Benki Bora kwa maendeleo endelevu, Benki Bora ya mwaka (AFAWA).
Tuzo hiyo ya Benki Bora kwa Wajasiriamali ilipokelewa na Afisa Mkuu wa Biashara, Boma Raballa, ambaye alieleza kuwa ushindi huo ni kielelezo cha dhamira ya Benki hiyo ya kuwapatia wateja na watanzania kwa ujumla wake huduma bunifu za fedha. Katika miaka 30 tokea kuanzishwa kwake, benki hiyo imeendelea kuwa nguzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wajasiriamali, hususan vijana na wanawake. “Ushindi huu si wetu pekee, bali ni wa jamii nzima tunayoihudumia,” ameeleza Raballa.
Benki ya CRDB imejidhihirisha kuwa mshirika mkubwa wa wajasiriamali nchini ikitoa uwezeshaji wa hadi shilingi bilioni 5. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2024 mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.2 imetolewa kwa zaidi ya wajasiriamali 230,000 kutoka sekta mbalimbali.
Benki ya CRDB imekuwa kinara katika huduma bunifu kwa wajasiriamali nchini, ikiwa Benki ya kwanza kuanzisha kitengo maalum kwa ajili ya kuhudumia kundi hili la wateja mwaka 2000.
Mwaka 2024, Benki ya CRDB ilifanya maboresho makubwa ya akaunti ya wajasiriamali ‘Biashara Akaunti’, ikiboresha pia fursa za uwezeshaji kupitia mikopo, pamoja na kutoa suluhisho za kidijitali kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa upokeaji malipo kwa wateja kupitia huduma za ‘LIPA HAPA’ na mashine za manunuzi (PoS).
Aidha, Benki hiyo pia inazo bidhaa mahususi kwa ajili ya kusaidia wafanyabiashra wanaogaiza bidhaa nje ya nchi kama ‘Mkopo wa Komboa,’ ukisaidia wateja kutoa mizigo yao bandarini kwa wakati. Hatua ambayo imeondoa ucheleweshaji katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa sokoni.
Sambamba na huduma, Benki pia inatoa huduma za ufadhili wa biashara (trade finance) na ufadhili wa rasilimali (asset financing), ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa wateja katika kukuza na kuimarisha biashara zao.
Benki ya CRDB pia imekuwa ikiwapatia wajasiriamali uzoefu wa biashara kimataifa kwa kuwapeleka nchi mbalimbali duniani ili kuwapa fursa za kujifunza na kuongeza thamani kwenye biashara wanazozifanya, huku ikiwajengea uwezo wa kushindana katika masoko ya kimataifa. Hii ni hatua muhimu katika kukuza ushindani wa bidhaa na huduma za Kitanzania.
Aidha Benki ya CRDB imekuwa ikishirikiana kimakakati na tasisi za kimataifa zinazolenga kuwasaidia wajasiriamali kama vile AGF, PROPARCO, DFC, GuarantCo na GCF pamoja na taasisi za hapa nchini kama vile PASS na TADB. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Benki hiyo imeweza kukusanya zaidi ya Dola za Marekani Milioni 700, ikionyesha imani ya washirika wa kimataifa katika uwezo na utayari wa benki katika kuwawezesha wajasiriamali nchini.
“Katika miaka 30 ya uwepo wetu, tumejifunza kuwa hakuna maendeleo ya kweli bila kuwainua wajasiriamali. Tunaendelea kujipanga kufikia wengi zaidi kupitia mikakati madhubuti ya ujumuishi, hasa kwa wanawake na vijana, kama sehemu ya kusaidia ajenda ya serikali ya maendeleo jumuishi,” aliongeza Raballa.
Tuzo hii ni ushahidi mwingine wa jinsi Benki ya CRDB imejikita kwa dhati katika kuwa daraja la mafanikio kwa maelfu ya wajasiriamali nchini. Kuelekea mbele, Benki hiyo imeendelea kuonyesha utayari wake katika kuwahudumia wajasiriamali kwa kutoa kipaumbele kikubwa kwa kundi hilo la wateja katika Mkakati wake wa Muda wa Kati wa Biashara wa 2023 – 2027.