Na Mwandishi Wetu, Nyasa
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, ‘Mitano Tena’ ni kwa mgombea urais, Dk. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza wake, Dk. Emmanuel Nchimbi, lakini wabunge na madiwani wasubiri kuchujwa kupitia vikao vya Chama.
Ameeleza hayo leo Juni 11, 2025 alipokuwa akizungumza katika kikao cha ndani kilichohusisha viongozi wa CCM Wilaya ya Nyasa, katika mji wa Mbamba Bay mkoani Ruvuma ambako anaendelea na ziara ya kuimarisha Chama.
“Niwaambie wana CCM wenzangu tunaposema mitano tena ni kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya urais na mgombea mwenza wake Dk. Emmanuel Nchimbi lakini kwa wabunge na madiwani wasubiri mchujo ndani ya Chama na mwaka huu tumeongeza idadi ya wapiga kura. Kwa mfano hapa Nyasa walikuwa wapigakura za maoni 900 lakini sasa wako 1,3000.”
Wasira alisema kupata wagombea safi ndani ya Chama wa udiwani na ubunge ni vema wakachaguliwa kwa utaratibu wa haki huku akisisitiza ‘mitano tena’ sio kwa watu wote ”Sio kila mtu ni mitano tena bali mitano tena ni kwa Rais Samia, wengine tunachujana.”
Akifafanua zaidi, Wasira alisema mabalozi wa CCM wana kazi ya kuchagua wagombea safi kupitia kura za maoni ambao watauzika mbele ya wananchi na sio wagombea ambao wanatokana na kununua kura.
“Heshima ya wajumbe ni anayesikiliza watu walionyuma yake, ni kupiga kura kwa mtu ambaye wananchi wanamtaka na katika majina matatu ambayo yatapendekezwa kupitia kura za maoni atapatikana mmoja ambaye atakuwa diwani au mbunge kwa miaka mitano.
“Kuna diwani amesema hapa kuwa wamefanya kazi nzuri na wanaomba ruhusa waendelee. Hakuna mtu anakataa ruksa lakini ruhusa haitolewi na mimi bali inatolewa na wananchi waliokupigia kura. Mimi nikimaliza (ziara) naondoka lakini wapigakura wanabaki na ndio watasema diwani amefanya kazi nzuri tunataka arudi na wale wapigakura wa kata yako watasema hivyo ndivyo.”