WAZIRI wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe, akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 11,2025 jijini Dodoma kuelekea katika uzinduzi wa kiwanda cha uzalishaji wa Mbolea cha ITRACOM Fertilizers Ltd kilichopo Nala, jijini Dodoma.
WAZIRI wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe, akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 11,2025 jijini Dodoma kuelekea katika uzinduzi wa kiwanda cha uzalishaji wa Mbolea cha ITRACOM Fertilizers Ltd kilichopo Nala, jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan,anatarajiwa kuzindua kiwanda cha uzalishaji wa Mbolea cha ITRACOM Fertilizers Ltd kilichopo Nala, jijini Dodoma pamoja na kuweka jiwe la msingi, kupanda miti kama ishara ya kukuza mazingira na kilimo endelevu, kukagua miundombinu ya kisasa ya Kiwanda hicho.
Hayo yameelezwa leo Juni 11,2025 na Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea katika uzinduzi wa kiwanda hicho utakaofanyika Juni 28 mwaka huu ambapo Kauli mbiu ya hafla hiyo ni “Kilimo ni Mbolea na Mbolea ni FOMI”.
Amesema kuwa Kiwanda hicho kimeweza kuajiri watumishi wapatao 1805. Ajira zisizokuwa za moja kwa moja zinazotokana na kiwanda kuwepo zinakadiriwa kuwa zaidi ya 5,000. Kiwanda kinatazamia kuajiri watu zaidi ya 3,000 na kuwa na ajira zisizokuwa za moja kwa moja zaidi ya 15,000.
‘Ujenzi wa Kiwanda hicho ulianza mwaka 2021 ambapo kina uwezo wa kutengeneza aina mbalimbali za mbolea kutegemeana na aina za udongo na mazao. Kwa sasa kimeshasajili aina 14 za mbolea, zinazotumika kwa mazao yote yanayolimwa Tanzania. Kiwanda pia kinazalisha chokaa-kilimo kwa ajili udongo ulioathirika na tindikali. “amesema Mhe.Bashe
Aidha amesema kuwa Mbolea aina za Fomi Otesha, Fomi Kuzia na Fomi Nenepesha zilianza kuingia sokoni Mwezi Desemba 2022 ambazo hutumika kuboresha afya ya udongo na kuongeza mavuno kwenye mazao ya chakula na biashara.
Uzinduzi huo pia utahudhuriwa na Waheshimiwa Marais wa nchi jirani akiwemo Mhe. Meja Jenerali (Mst) Evariste Ndayishimiye, Rais wa Jamhuri ya Burundi; na Viongozi Wakuu wa Serikali wakiwemo Mawaziri wa Kilimo kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiongozwa na Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Mhe. Hussein Bashe (Mb); Makatibu Wakuu; Wakuu wa Mikoa; Wakuu wa Wilaya na Wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani.