Na Khadija Kalili, Michuzi Tv
VIONGOZI na wanachama wa taasisi ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi Tanzania TAWEN wametakiwa kuwekeza elimu kwa mtoto wa kike kwa sababu elimu ni silaha ya kwanza ya kumuwezesha mwanamke kusimama , kujisimamia na kuongoza kwa ujasiri na weledi.
“Sambamba na hilo ili tuweze kufikia malengo hayo tunayoyatarajia hatuna budi kwa umoja wetu sote kupambana na kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto hususan kipindi hiki ambacho kinaripoti matukio mengi ya ukatili kwa watoto kama kubakwa, kulawitiwa, ndoa za utotoni, mimba za utotoni, familia kutelekeza watoto , ajira za watoto na watoto wengi kukosa haki ya kupata elimu”.
Hayo yamesema na Afisa Utumishi Mwandamizi Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani Emmanuel Lweyo alipokuwa mgeni rasmi katika mafunzo ya uongozi kwa wanachama wa Taasisi ya Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi Tanzania (TAWEN) iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Sports Lounge Kibaha Mkoani Pwani tarehe 9 Juni 2025.
Lweyo amesema kuwa ni muhimu kuwa na mazingira rafiki kwa wanawake anaotaka kuingia kwenye uongozi ikiwemo sera zinzolinda haki zao nafasi za uwakilishi wa lzima na kuondoa ubaguzi wa kijinsia.
“Jamii zetu lazima zibadilike mtazamo wa kwamba mwanamke hawezi kuwa kiongozi huu ni mzigo wa fikra potofu ambaom tunapawa kuuangusha kwa nguvu ya elimu, mazungumzo ya wazi na mfano bora kutoka kwa wanawake waliopiga hatua na mfano mzuri kwa nchi yetu ni Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan , Spika wa Bunge la Tanzania na Spika wa Mabunge Duniani Mhe. Dkt. Tulia Ackson na wengine waliopata nafasi za juu za uongozi wa taifa letu” amesema Lweyo.
“Katika historia ya jamii nyingi wanawake wamekuwa wakionekana kama wapishi wa familia walezi wa watoto na wasaidizi wa waume zao lakini ukweli ni kwamba wanawake ni zaidi ya hayo, mwanamke ana uwezo wa kuongoza ,kupanga, kuamua na kuleta mabadiliko makubwa katika familia , jamii, taifa na hata dunia kwa ujujmla”amesema Lweyo.
Katika dunia ya leo hatuwezi tena kuzungumzia maendeleo bila kuhusisha wanawake , hatuwezi tena kupanga sera kuendesha siasa au kusimamia uchumi kwa mafanikio bila ushiriki wa kina wa wanawake katika nafasi n za uongozi.
Lweyo amesisitiza kwa kusema kuwa “tunahitaji wanawake katika nyanja za kisasa katika bodi za mashirika kwenye uongozi wa shule , taasisi za kifedha na kwenye nyanja zote za maisha”amesema Lweyo.
Akimnukuu Hayati Nelson Mandela ” Elimu ni silaha yenye nguvu zaidi unavyoweza kuitumia kubadilisha dunia” tukimpa mwanamke elimu na nafasi ya kuongoza tutakuwa tumebadilisha dunia si kwa maneno bali kwa vitendo.
Kwa hiyo leo tunapozungumza juu ya mustakabali wa taifa letu tusisahau kwamba maendeleo ya kweli hayaji bila usawa wa kijinsia , kukuza uongozi wa wanawake si hisani ni haki , si chaguo ni wajibu na siyo kwa faida ya wanawake pekee bali kwa faida ya ya kizazi chote .
Taifa linalothamini na kujali ndoto na makuzi ya watoto ndilo taifa hai kwa kuwa watoto ndiyo nguvukazi , viongozi na wabeba maono ya taifa la baadaye hivyo ni wajibu wetu sote kuwalea katika maadili mema kuwalinda na kuwapatia haki zao za msingi ili tupate Taifa lililo bora.
Viongozi wengine wa TAWEN waliohudhuria mafunzo hayo ni Mwenyekiti Florence Masunga , Katibu Dafroza Mzava, Afisa Miradi Asha Baraka Mwenyekiti wa Vijana TAWEN Cosmas Ikwabe na Mwenyekiti wa Umoja Wa Wanawake Wilaya ya Kibaha (UWT)