
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga kutoa uamuzi Aprili 28, 2025 kwa njia ya mtandao kuhusu pingamizi la kisheria lililowasilishwa na mawakili wa utetezi wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, katika kesi ya uchochezi inayomkabili.
Katika kile kilichoonekana kuwa siku yenye mijadala mizito, kesi hiyo ilisikilizwa leo kwa njia ya mtandao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, lakini ilikumbwa na sintofahamu baada ya Lissu kugoma kusomewa maelezo ya awali kwa njia ya mtandao.
KILICHOTOKEA SIKU YA LEO MAHAKAMANI:
- Mawakili wa Serikali walitarajia Lissu asomewe Maelezo ya Awali (PH), lakini Lissu hakuonekana kwenye mtandao.
- Askari Magereza aliyehojiwa na Hakimu alisema kuwa Lissu amegoma kusomewa kwa njia ya mtandao.
- Hata hivyo, Hakimu Mhini aliruhusu mchakato wa kesi kuendelea licha ya Lissu kutokuwepo machoni pa mahakama kwa njia ya visual.

HOJA ZA MAWAKILI WA LISSU
Lissu anatetewa na jopo la mawakili 31 wakiongozwa na Wakili Mpale Mpoki, wakisaidiana na Peter Kibatala, Alute Mugwai na Jeremiah Ntobesya. Jopo hilo limewasilisha pingamizi likidai kuwa:
“Kesi ya uchochezi haiwezi kuendelea kwa njia ya mtandao bila mshtakiwa kuwepo mahakamani kimwili na kusaini maelezo ya awali kama inavyotakiwa kisheria.”
Mawakili wa utetezi wamesisitiza kuwa haki ya mshtakiwa haiwezi kutekelezwa ipasavyo kwa njia ya mtandao, hasa kwa hatua ya kusomewa maelezo ya awali.
Hakimu Mhini ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 28, 2025, ambapo atatoa uamuzi iwapo Lissu atatakiwa kufikishwa mahakamani au kesi hiyo itaendelea kwa njia ya mtandao.
Huku kesi ya uchochezi ikisubiri hatma, kesi ya uhaini inayomkabili Lissu inaendelea kusikilizwa, ikionyesha kuwa kiongozi huyo mkuu wa upinzani bado yupo kwenye mchakato mzito wa kisheria.