Na Meleka Kulwa, Dodoma
DODOMA, Juni 11, 2025 – Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji inatarajiwa kuwasilisha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha ujao, ikiwa ni mara ya kwanza bajeti hiyo kugharamiwa kwa asilimia kubwa na fedha za ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema kuwa bajeti hiyo ni ya kihistoria na ya kipekee kwani inatoa mwelekeo wa bajeti ya uchaguzi wa mwaka 2025.
“Hii ni bajeti ya mwisho ya Serikali ya Awamu ya Sita na itakuwa ya kipekee kwa sababu asilimia kubwa ya fedha zinatokana na mapato ya ndani. Ni muhimu wananchi waipe uzito na kuifuatilia kwa karibu,” alisema Msigwa.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Awamu ya Sita imepiga hatua kubwa kiuchumi baada ya kupokea gawio la jumla ya shilingi trilioni 1.28 kutoka mashirika ya umma, ikiwa ni matokeo ya ufanisi wa uwekezaji wa shilingi trilioni 86.
Msigwa alisema kuwa mafanikio hayo ni matunda ya utekelezaji wa falsafa ya 4R (Reconciliation, Reforms, Resilience, and Rebuilding), iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuongeza kuwa gawio hilo linatarajiwa kuongezeka kila mwaka kutokana na mikakati madhubuti iliyowekwa.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali, Msigwa alisema kuwa Awamu ya Pili ya ujenzi huo imekamilika kwa asilimia 90.1. Mradi huo unajumuisha jumla ya majengo 34, ambapo sita kati yake tayari yanatumika, huku gharama zake zikifikia shilingi bilioni 738.9.
Aidha, miundombinu mingine inaendelea kujengwa ikiwemo barabara za lami zenye urefu wa kilomita 59.1 na umeme wa chini ya ardhi wa kilomita 42. Zaidi ya miti 233,000 imepandwa katika maeneo ya wazi na pembezoni mwa barabara, ikiwa ni juhudi za serikali katika kulinda mazingira.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku saba kuanzia Juni 15, katika mikoa ya Simiyu na Mwanza. Katika ziara hiyo, Rais atazindua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kufungua rasmi Daraja la Kigongo-Busisi ambalo limekamilika kwa asilimia 100,” Amesema Msigwa.
Msigwa alibainisha kuwa Rais pia amepokea mwaliko wa kufanya ziara rasmi katika nchi ya Msumbiji pamoja na Visiwa vya Comoro, hatua inayoashiria mahusiano imara ya kimataifa.
Katika mkutano huo, Msigwa aliwaasa vijana, hususan wa vyuo vikuu, kutumia mitandao ya kijamii kwa tija na kwa kujenga taifa badala ya kuichafua serikali. Alikumbusha kuwa sheria dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ipo na vyombo vya dola vitaendelea kuchukua hatua kwa wanaovunja sheria hizo.