NA DENIS MLOWE, IRINGA
MWENYEKITI Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kanda ya Iringa, Moses Ambindwile, amewataka wenyeviti wa mitaa na watendaji wa kata kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na mipaka ya madaraka yao ili kuepuka migogoro ya kisheria inayoweza kuathiri nafasi zao za uongozi katika jamii wanayoongoza.
Akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi hao yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa TLS na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ambindwile alisema utawala bora hujengwa juu ya nguzo kuu nne ambazo ni uwazi, uwajibikaji, ushirikishwaji na ufuataji wa sheria.
Alisema kuwa Kiongozi unapoongoza bila kufuata sheria unajiweka kwenye mtihani mkubwa na kuna uwezekano ikakuondolea na ikakuharibia heshima.
Aliongeza kuwa licha ya kukumbana na changamoto hizo inaweza inaweza kukuondoa kabisa kwenye nafasi yako ya madaraka katika utendaji.
Wakili Ambindwile aliwasisitiza wenyeviti na watendaji kutambua mipaka yao na kujiepusha na maamuzi ya kibinafsi yanayokiuka utaratibu, kanuni na sheria za nchi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Iringa, Loveness Maingu alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakitoa barua za dhamana kwa watu wanaotuhumiwa kwenye kesi nzito za kijamii bila kujiridhisha kama wanawafahamu na kama kweli wanaishi kwenye maeneo yao.
“Kuna wenyeviti wanaandika barua za dhamana bila hata kuweka kumbukumbu wala namba za nyumba. Wengine wanawapa watu ambao si wakazi wa mitaa yao kwa tamaa ya kupokea ‘kitu kidogo.’ Hili halikubaliki. Ni hatari kwa usalama wa jamii,” aliongeza.
Alisema dawati hilo liliundwa ili kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia, huku akieleza kuwa kundi la madereva bodaboda na bajaji limeonekana kuhusika zaidi katika ukatili wa kingono kwa watoto wa kike.
“Tunapokea watoto waliobakwa na kulawitiwa na baadhi ya madereva hawa. Wenyeviti tafadhali fuatilieni mienendo yao. Hawa ni watu mnaoishi nao mitaani. Wengine wanazunguka kama watu wema kumbe wanaficha uhalifu mkubwa,” alionya.
Aliwataka wazazi, hasa akina mama, kupunguza ulevi na kurejesha maadili katika familia kwa kuwa changamoto kubwa sasa ni watoto kulelewa hovyo na kukosa mwelekeo.
“Watoto hawaelekezwi tena kwenda misikitini wala makanisani. Wanalelewa mitaani, bila maadili. Mtoto wa aina hii anaweza kuwa mbakaji, mwizi au hata muuaji wa mzazi wake,” alisema kwa masikitiko.
Aidha, Maingu aliwashauri viongozi kuendelea kuwakumbusha watoto katika mikutano ya mitaa na kata kuchukua namba za usajili za pikipiki au bajaji wanazopanda, ili iwe rahisi kufuatilia iwapo kutatokea tukio la ukatili.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Lubida, Demitilio Stephan Matandula, aliainisha changamoto wanazokumbana nazo katika kuwahudumia waathirika wa ukatili wa kijinsia, ikiwemo gharama za kuwasafirisha polisi na hospitali, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya jamii na mamlaka husika.
Alisema mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwao na akaomba yaendelezwe ili kusaidia viongozi wengi zaidi kupata maarifa ya kisheria.
“Tunaomba elimu hii iendelee. Inatusaidia sana kujua wapi mipaka yetu ya kiutendaji ipo na namna ya kutatua migogoro bila kuingia matatani,” alisema Matandula.
Mmoja wa wanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Nicholaus Nshashi, alisema kwa kushirikiana na TLS imeamua kuwekeza kwenye elimu kwa viongozi wa mitaa ili kuongeza ufanisi katika kushughulikia changamoto zinazoikabili jamii kwa kutumia sheria, kanuni na miongozo husika.
Kwa pamoja, wadau hao walisisitiza kuwa iwapo viongozi wa chini wataelewa majukumu yao kwa kina na kuzingatia sheria, jamii itapata mafanikio makubwa katika vita dhidi ya ukatili, migogoro ya ardhi, na ulinzi wa haki za watoto na watu wenye ulemavu.