Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Charles Mahera,akizungumza jijini Dodoma wakati wa Kongamano la Pili la Sayansi ya Afya (UDOM Scientific Conference on Health – USCHe 2025), kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka,akizungumza jijini Dodoma wakati wa Kongamano la Pili la Sayansi ya Afya (UDOM Scientific Conference on Health – USCHe 2025).
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Bw. Jabir Shekimweri,akizungumza jijini Dodoma wakati wa Kongamano la Pili la Sayansi ya Afya (UDOM Scientific Conference on Health – USCHe 2025).
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe,akichangia mada wakati wa Kongamano la Pili la Sayansi ya Afya (UDOM Scientific Conference on Health – USCHe 2025).
Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Charles Mahera (hayupo pichani) wakati wa Kongamano la Pili la Sayansi ya Afya (UDOM Scientific Conference on Health – USCHe 2025).
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Charles Mahera,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Kongamano la Pili la Sayansi ya Afya (UDOM Scientific Conference on Health – USCHe 2025), kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko.
Na.Meleka Kulwa-DODOMA
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Charles Maher, amesema Serikali imenufaika kwa kiasi kikubwa na tafiti za kisayansi katika kutatua changamoto za sekta ya afya nchini.
Dkt.Mahera ameyasema hayo jijini Dodoma, wakati wa Kongamano la Pili la Sayansi ya Afya (UDOM Scientific Conference on Health – USCHe 2025), kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko,amesema kuwa makongamano ya kisayansi ni jukwaa muhimu linalowezesha Serikali kupokea maoni na mapendekezo ya kitaalamu kutoka kwa watafiti na wanazuoni wa ndani ya nchi.
“Makongamano kama haya yanaiwezesha Serikali kuandaa sera na mikakati ya afya inayotegemea ushahidi wa kisayansi. Ni muhimu tafiti hizi zitumike ipasavyo kwa manufaa ya jamii yetu,” alisema Dkt. Mahera
Kongamano hilo limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia Shule Kuu ya Tiba na Afya ya Kinywa (SoMD) na Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii (SoNPH), likiwa ni sehemu ya mikakati ya kukuza tafiti za afya na kuimarisha mchango wa taaluma katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya. Alisema UDOM ina wajibu wa kuhakikisha inazalisha wataalamu bora kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
“Kongamano la kisayansi lina umuhimu mkubwa kwa taifa. Tafiti zetu zisitumike na mataifa mengine kutengeneza bidhaa na sisi tuje kununua. Ni lazima tuyatumie matokeo ya tafiti kujinufaisha sisi wenyewe,” alisema Prof. Kusiluka.
Aliongeza kuwa, sambamba na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, ni muhimu tafiti zijielekeze pia kwenye ajali za barabarani ambazo zimeendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo katika nchi zinazoendelea.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, alisema Wizara itaendelea kushirikiana na vyuo vikuu kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinatumika moja kwa moja katika uundaji wa sera na miongozo ya afya.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Bw. Jabir Shekimweri, alisema Serikali ya Mkoa itaendelea kushiriki na kuunga mkono makongamano ya aina hiyo, akisisitiza kuwa ni muhimu yawe endelevu kwa ajili ya kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali za kiafya zinazoikabili jamii.