Ruangwa, Lindi
Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ipo mbioni kukamilisha kiwanda cha kuchakata chumvi itakayozalishwa na wachimbaji wa chumvi katika mkoa wa Lindi na Mtwara.
Hayo yamebainishwa leo Juni 12, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva wakati akifungua mafunzo ya namna bora ya kuzalisha chumvi ambayo yanaenda sambamba na maonesho ya madini na fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini wilayani Ruangwa.
Mwanziva ameeleza kuwa, kutokana na umuhimu wa kiwanda hicho matarajio ni kwamba ifikapo mwezi Agosti 2025 kitakuwa kimekamilika na kuanza uchakataji mbalimbali ikiwa pamoja na kuiongezea thamani chumvi ghafi kutoka kwa wazalishaji.
Akibainisha kuhusu lengo la kufungua kiwanda hicho, Mwanziva amebainisha kuwa, Serikali imebaini changamoto zinazojitokeza kwa wazalishaji wa chumvi, huvyo imeona kuna kila sababu ya kufungua kiwanda kitakachopokea malighafi ya chumvi kutoka kwa wakulima na kuboresha kwa kuiongezea thamani ili zao hilo liwe na tija kwa wazalishaji na taifa kwa ujumla.
Mwanziva amefafanua kuwa, kiwanda hicho kitafanya kazi mbalimbali ikiwa pamoja na usafishaji na ufungaji wa chumvi, kitatoa mafunzo ya shamba darasa ili kujenga uwezo kwa wakulima wa chumvi pamoja na kununua chumvi ghafi kutoka kwa wazalishaji.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi (RMO) mkoa wa Mtwara Winfrida Mrema amesema kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa madini ya chumvi nchini hivyo kupitia mafunzo hayo, changamoto zote zilizotajwa zitawashirishwa kwa mamlaka husika ili kupata utatuzi wa haraka.
Naye, Mwakilishi kutoka Wizara ya Madini Mjiolojia Daniel Kidesheni amesema, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) litaendelea kufanya tathimini katika mashamba ya chumvi katika mikoa ya kusini ili kuendelea kufahamu hali halisi ya mashamba na kuwasilisha taarifa ili kuweka mikakati bora ya kuongeza thamani ya chumvi nchini.
Awali, akielezea kuhusu mwenendo wa uzalishaji chumvi nchini mwakilishi kutoka Chama cha Wazalishaji wa Chumvi Tanzani (TASPA) Ally Ismail , ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kulinda soko la ndani jambo ambalo limeongeza tija kwa wazalishaji ukilinganisha na kipindi cha miaka ya nyuma.
Pamoja na pongezi hizo , Ismail ameiomba serikali kupunguza gharama za uagizaji wa madini joto yanayotumika katika uboreshaji wa madini ya chumvi.
Kulingana na takwimu mahitaji ya chumvi nchini Tanzania ni tani 200,000 kwa mwaka.