Na WMJJWM, Tabora
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu amewataka waratibu wa Madawati ya Jinsia maeneo ya Umma kuwajibika na kutenda haki ili kuwa na jamii salama isiyo na vitendo vya ukatili.
Felister ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha mafunzo kwa waratibu wa madawati ya jinsia maeneo ya umma mkoani Tabora Juni 12, 2025 mafunzo ambayo yamewajumuisha washiriki kutoka mikoa ya Tabora, Songwe na Rukwa.
“Matukio haya ya ukatili tutayaondoa ikiwa wote tutazungumza sauti moja hivyo nawasihi tukatende haki, kila mmoja aone jukumu la kupinga vitendo vya ukatili ni lake” amesisitiza Naibu Katibu Mkuu Felister.
Ameongeza kwamba Jamii inatakiwa kufahamu na kufikisha taarifa za Ukatili wa kijinsia kwa maofisa wa Madawati yanayopatikana katika vituo vya Polisi na vituo vya mabasi na kwa maofisa Ustawi wa Jamii wanaopatikana katika halmshauri na Ofisi za Kata.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt. John Mboya ametoa pongezi kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha changamoto zozote za ukatili zinapotokea wanashughulika nazo na kuzipatia ufumbuzi.
“Sote ni Mashahidi wazuri kwa hii Wizara, kila tunapowafikia kwa changamoto yeyote wamekuwa na muitikio wa haraka na tunafanikiwa kutatua changamoto hiyo bila kuwekewa vikwazo vya ucheleweshwaji” ameleeleza Dkt. John
Amesisitiza kuwa wanaume wasione haya kuyatumia madawati hayo katika kutoa taarifa za ukatili ambayo sasa yamefika kwenye ngazi ya maeneo ya umma.
Awali wakati akitoa salama za Wizara Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia Rennie Gondwe amesema kuwa Serikali imefanya jitihada nyingi kuhakikisha vitendo vya ukatili vinatokomezwa ndani ya jamii na miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na uanzishwaji wa Madawati ya Jinsia katika maeneo mbalimbali.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kupitia idara ya Maendeleo ya Jinsia imepanua wigo wa madawati ya Jinsia ambapo jumla ya madawati 238 kwenye masoko ndani ya mikoa 19 tayari yameanzishwa na yanafanya kazi huku mafunzo mbalimbali ya namna bora ya uendeshwaji wa madawati hayo yamekuwa yakitolewa Mara kwa mara lengo ni jamii iwe na sauti moja ya kukemea, kupinga na kutotenda ukatili.