*Zaidi ya asilimia 95 ya ajira toka Sekta ya Madini zimekwenda kwa wazawa.
*Sekta ya Madini yafunganisha na Sekta nyingine za kiuchumi.
Ruangwa, Lindi
Imeelezwa kwamba, kwa kipindi cha Miaka Minne Sekta ya Madini mkoani Lindi imefanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia shighuli za uchimbaji na uwekezaji katika rasilimali madini mbalimbali zinazopatikana mkoani humo yakiwemo madini ya kinywe, dhahabu, jasi, shaba, madini ya vito na madini ujenzi.
Hayo, yameelezwa leo Juni 11, 2025 na Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe.Shaib Kaduara wakati akifungua maonesho ya madini na fursa za uwekezaji mkoani Lindi.
Mhe. Kaduara amesema kuwa, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2022/2023, Lindi ilikusanya mapato ya Serikali kiasi cha shilingi bilioni 4.33 kutoka kwenye madini, ikiwa ni asilimia 90.42 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 4.8 ambapo kiwango hiki kinadhihirisha kuwa bado kuna fursa kubwa ya kuongeza mapato kupitia uwekezaji zaidi na matumizi bora ya rasilimali madini.
Akielezea kuhusu mikakati ya kuendeleza Sekta ya Madini nchini, Kaduara ameeleza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo na mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa viwanda vya kusafisha na kuchakata madini hususan madini mkakati na madini adimu ili kuyaongezea thamani madini hayo kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack amesema kuwa, miradi mikubwa ya uchimbaji madini inachangia kwa kiasi kikubwa katika mageuzi ya kiuchumi ndani ya mkoa, akitolea mfano madini ya kinywe yanayokadiliwa kuwa na tani milioni 17, ambapo yakivunwa yatachangia takribani dola bilioni 12.
Akielezea kuhusu maendeleo ya mwenendo wa leseni za uchimbaji na utafiti zilizopo mkoani humo, Telack amesema kuwa, awali kulikuwa na leseni za wachimbaji wadogo 2811 ila kwa sasa zipo 3218, leseni za Kati zimeongezeka kutoka 16 hadi 25, leseni kubwa 1 na leseni za uchenjuaji zipo 10.
Kuhusu fursa za ajira, Talack amebainisha kuwa, kupitia miradi mikubwa ya uchimbaji madini ya kinywe , kama vile Lindi Jumbo , unatarajiwa kuajiri zaidi ya watu 350.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt.Venance Mwase ameupongeza Mkoa wa Lindi kwa juhudi mbalimbali za kuendeleza Sekta ya Madini hasa kwenye madini mkakati ambapo amehaidi kuwapatia wachimbaji wadogo mashine ya kuchoronga miamba ili vikundi vilivyopo vichimbe kwa tija.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Mwase amesema STAMICO itaendelea kutoa mafunzo ya shamba darasa kwa wakulima wa chumvi kwa lengo la kufahamu namna bora ya kuchakata zao la chumvi pamoja na kuwaunganisha na masoko.