Songea, Ruvuma – Juni 12, 2025
Afisa Tehama kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Alfa Makaya, amesema kuwa ni muhimu kwa kila mtu kulinda simu yake kwa kuweka nywila (password) thabiti, kwani kufanya hivyo si hiari bali ni wajibu wa kisheria unaolenga kulinda faragha ya mtu binafsi.
Amesema kuwa sheria za mawasiliano nchini zinakataza mtu yeyote kuingilia mawasiliano ya mwingine, ikiwemo ya mwenza au mwanafamilia. Aidha, ametahadharisha kuwa endapo kuna matatizo ya kifamilia au binafsi, ni vyema kutumia njia rasmi za usuluhishi badala ya kuvunja haki ya faragha kwa kupekua simu ya mtu mwingine.
Makaya amehimiza Watanzania kuhakikisha simu zao zina nywila ili kulinda taarifa binafsi pindi simu inapopotea au kuibiwa, jambo ambalo pia linaongeza usalama wa taarifa za mtumiaji.
Akizungumzia maendeleo ya mawasiliano katika Mkoa wa Ruvuma, Makaya amesema kuwa zaidi ya laini milioni mbili za simu zimesajiliwa mkoani humo, ameeleza kuwa ongezeko hilo limechangia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta mbalimbali za uchumi wa kidigitali ikiwemo mawasiliano, elimu, afya, pamoja na kilimo, ametoa mfano wa matumizi ya teknolojia ya kisasa kama ndege zisizo na rubani (drone) katika shughuli za umwagiliaji mashambani.
Kwa upande wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano, Makaya ameeleza kuwa TCRA imefanya ziara katika zaidi ya vijiji 580 vya Mkoa wa Ruvuma na kubaini kuwa huduma ya mawasiliano imewafikia wananchi wa maeneo hayo, hata hivyo alifafanua kuwa si mitandao yote ya simu inayopatikana kwa pamoja katika kila kijiji, lakini angalau kuna mtandao mmoja unaopatikana katika kila eneo ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayekosa huduma.
Pamoja na mafanikio hayo, Makaya amesema kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya watu kusambaza jumbe za kitapeli, hasa zile zinazohamasisha kutuma ujumbe kwa namba fulani kwa lengo la udanganyifu, amesema TCRA inaendelea kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo na amewataka wananchi kuripoti matukio kama hayo kupitia namba 15040 ili kuvisaidia vyombo husika kutokomeza kabisa matukio hayo.
Kwa muktadha huo, TCRA inaendelea kuhimiza wananchi kuzingatia matumizi salama ya simu na teknolojia ya mawasiliano kwa kulinda taarifa binafsi, kuheshimu faragha za wengine, na kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya uhalifu wa mtandaoni.
Kulinda simu kwa nywila, kuripoti vitendo vya kitapeli, na kutumia huduma za mawasiliano kwa njia sahihi ni hatua muhimu katika kujenga jamii salama, inayonufaika kikamilifu na uchumi wa kidigitali, ushirikiano wa kila mmoja ni nguzo muhimu kufanikisha mawasiliano bora kwa maendeleo ya Taifa.