Kati kati ni Meneja wa Kitengo cha Ulipaji kodi kwa hiari na ufatiliaji (Compliance and Enforcement) kutoka TRA, Bashiru Kahenaki akizungumza na wafanyabiashara wakati katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Juni 12, 2025 Kulia ni Meneja wa Ritani kutoka Idara ya walipa kodi wa kati kutoka wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Sandey Kayombo na kushoto ni Jacqueline Mawole kutoka kampuni ya Intertek Caleb Brelt Tanzania LTD
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewahakikishia wafanyabiashara kuwa lengo lake si kukwamisha biashara, bali kuwawezesha wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao huku wakitimiza wajibu wa kulipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja na walipakodi wa kati, Bashiru Kahenaki, Meneja wa Kitengo cha Ulipaji kodi kwa hiari na ufatiliaji (Compliance and Enforcement) kutoka TRA, amesema kuwa mamlaka hiyo ipo kwa ajili ya kusaidia wafanyabiashara kufanikisha shughuli zao kwa kufuata utaratibu sahihi wa ulipaji kodi.
“TRA tupo sio kukwamisha biashara, tupo kuunga mkono hizi biashara ziweze kuendelea. Wanapokuwa na changamoto, tumewaelekeza njia sahihi za kupita, lakini pia kuwaambia tupo kwa ajili yao na kwamba wana nafasi mbalimbali za kuelezea changamoto wanazopitia,” alisema Kahenaki.
Mkutano huo uliandaliwa kwa lengo la kujadili njia bora za kuboresha ukusanyaji wa kodi sambamba na kuweka mazingira bora ya kufanikisha biashara nchini. Pia, mkutano huo ulitumiwa kuwapongeza walipakodi kwa juhudi zao ambazo zimeiwezesha TRA kuongeza mapato ya nchi na kuiwezesha serikali kutoa huduma kwa wananchi.
“Tumeweza kujadili mambo mengi kwa pamoja, lakini pia umekuwa mkutano mzuri wa kusikiliza changamoto wanazozipitia walipakodi na kuweza kuzitatua,” ameongeza Kahenaki.
Mohamed Remtulla, mmoja wa walipakodi wa kati waliokuwa kwenye mkutano huo, aliipongeza TRA kwa kuwaita wafanyabiashara kuelezea changamoto zao, jambo alilosema linaonesha ushirikiano na dhamira ya kuboresha mazingira rafiki ya biashara.
“Kuna vitu vingi tumejifunza na tunayo matumaini makubwa kwamba changamoto tulizoeleza zitaenda kufanyiwa kazi mara baada ya kikao hiki,” amesema Remtulla.
Kwa upande wake, Jacqueline Mawole kutoka kampuni ya Intertek Caleb Brelt Tanzania LTD ameeleza kuwa kikao hicho kimemsaidia kufahamu njia sahihi za kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika shughuli zake za kikodi.
“Kupitia kikao cha leo nimeweza kujua nini ninachotakiwa kufanya nikiwa kama mlipakodi,” amesema Jacqueline.
TRA imeendelea kusisitiza kuwa ipo tayari kushirikiana na walipakodi kwa kuwapatia elimu, mwongozo, na majibu kwa changamoto wanazokutana nazo ili kuhakikisha mazingira bora ya biashara na ulipaji kodi nchini.
Matukio mbalimbali katika mkutano kati ya walipakodi wa kati na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Picha ya pamoja.