Na, WAF-Dodoma
Serikali imetoa wito kwa wananchi kubadilika na kuwekeza katika bima ya afya kama njia ya kujiandaa na changamoto za kiafya, ikiwemo gharama kubwa za matibabu ya magonjwa kama saratani.
Wito huo umetolewa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, alipokuwa akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mhe. Ester Matiko (Viti Maalum), ambaye alitaka kufahamu kama Serikali haioni haja ya kuweka kifurushi cha saratani kwenye bima ya afya ya chini ili kuwezesha wananchi wa kawaida kupata huduma, kutokana na gharama kubwa za matibabu ya ugonjwa huo.
Akijibu swali hilo, Dkt. Mollel amesema jamii inapaswa kubadilika na kuwekeza kwenye bima ya afya ili kuimarisha afya zao.
“Watu wako tayari kuchangisha Milioni 100 kwa ajili ya harusi, lakini mtoto anapozaliwa hakuna anayechangia hata kwa ajili ya matibabu. Hii inaonyesha kwamba jamii inathamini sherehe kuliko afya,” amefafanua Dkt. Mollel.
Aidha, Dkt. Mollel amebainisha kuwa Serikali imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 200 kwa ajili ya msamaha wa matibabu, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha wananchi, hususan wasio na uwezo, wanapata huduma za afya bila vikwazo vya kifedha.
Naibu Waziri amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya bima ya afya ili kuhakikisha huduma za afya, zikiwemo za magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, zinapatikana kwa wote kwa gharama nafuu kupitia mfumo wa bima ya afya kwa wote unaotarajiwa kuimarika zaidi katika utekelezaji wa sera mpya ya afya.