Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Omari Kipanga,akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kituo cha Huduma kwa wateja “Contact center” hafla iliyofanyika leo Juni 12,2025 katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imezindua Kituo cha Huduma kwa wateja “Contact center” kilichograimu takribani Milioni Mia Moja chenye lengo la kuanza kupokea ushauri,maoni na mawazo ya watu mbalimbali ili kuhakikisha wizara hiyo inaendelea kuboresha sekta ya elimu.
Kituo hicho kimefadhiliwa kwa kiasi kikubwa na serikali ya Uingereza kupitia ofisi yake ya Commonwealth na mradi wa shule bora
Akizungumza jijini Dodoma baada ya kuzindua Kituo hicho Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Omari Kipanga, amesema kuwa kupitia kituo hicho anaamini wataweza kushughulikia changamoto mbalimbali ambazo zipo katika Wizara hiyo.
“Kupitia kituo hichi tutaenda kutatua changamoto pamoja na kwenda kufanya kazi kwa weledi lengo letu tunataka wizara yetu izidi kusonga mbele katika masuala ya elimu,”amesema Kipanga
Aidha amesema kuwa Serikali kupitia wizara hiyo iliona ni muhimu kuwa na kituo hicho ili kuanza kupokea ushauri,maoni na mawazo ya watu mbalimbali ili kuhakikisha wanaendelea kuboresha elimu na kuweza kuwa na elimu ambayo Rais Dk. Samia anaitaka ya ulimwengu jinsi inavyokwenda.
“Kipekee niwashukuru na kuipongeza serikali ya Uingereza kwa kukiboresha kituo hiki kutoka Call Center hadi Contact Center na sisi tunaahidi tutatunza vifaa walivyowezeshwa,” ameeleza
Hata hivyo amesema kuwa watanyakazi wa Kituo hicho tayari wameshapata mafunzo na wana amini watafanyakazi kwa weledi kuhakikisha wanawahudumia watanzania.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Carolyne Nombo,amesema kuwa kituo hicho wamekisubiri kwa muda wa miaka miwili na sasa kimekamilika.
“Kupitia kituo hiki tunaenda kuwasiliana na wananchi katika maboresho ya elimu, Wizara itaenda kutunza kituo hiki na kuhakikisha kwamba huduma ambazo zinatolewa zitakuwa bora na katika miaka ijayo,” amesema Prof.Nombo
Kwa upande wake Mwakilishi wa Ubalozi wa Uingreza Dkt.John Lusingu,ametoa wito kwa watendaji wa wizara hiyo kutekeleza maoni ya wananchi.











