Mkurugenzi wa Tafiti, Miungano ya Makampuni na Uraghibishi Tume ya Ushindani (FCC) B. Zaytun Kikula akizungumza na Wanawawake Wajasiriamali Mkoa wa Dar es Salaam wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo kuhusu Uhamasishaji wa masuala ya ushindani, kumlinda mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia iliyofanyika leo Juni 13, 2025 katika Ukumbi wa Ofisi za FFC , Dar es Salaam. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Makamu wa Rais wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Mwalongo Kambewe akitoa neno la shukrani katika semina ya kuwajengea uwezo Wanawawake Wajasiriamali Mkoa wa Dar es Salaam KUHUSU Uhamasishaji wa masuala ya ushindani, kumlinda mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia iliyoandaliwa na FCC.
Wanawawake Wajasiriamali Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa wa Tume ya Ushindani (FCC) baada ya ufunguzi semina ya kuwajengea uwezo kuhusu Uhamasishaji wa masuala ya ushindani, kumlinda mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia iliyofanyika leo Juni 13, 2025 katika Ukumbi wa Ofisi za FFC , Dar es Salaam.
……………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Tume ya Ushindani wa Haki (FCC) imeendesha mafunzo maalumu kwa wajasiriamali wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu namna bora ya kulinda biashara zao, kuwahudumia wateja kwa ubora, na kuhimili ushindani katika soko.
Akizungumza leo, Juni 13, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Utafiti, Muungano na Utetezi wa FCC, Bi. Zaytun Kikula, amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha mazingira ya biashara na kuwawezesha wanawake kuchangia kikamilifu maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Bi. Kikula amesema kuwa wanawake wajasiriamali wana mchango mkubwa katika ustawi wa familia, jamii, na uchumi kwa ujumla, hivyo kuwawezesha ni hatua muhimu katika kuleta maendeleo ya kitaifa.
“Jukwaa hili linatupa fursa ya kuzungumza moja kwa moja na wamiliki wa biashara, kuwapatia elimu kuhusu sheria za ushindani, na kuwasaidia kujenga biashara imara na endelevu,” amesema Bi. Kikula.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), Bi. Mwalongo Kambewe, amewahimiza washiriki wa mafunzo kutumia maarifa waliyojifunza kuboresha biashara zao na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Naamini wanawake walioshiriki mafunzo haya wataona mabadiliko makubwa si tu kwenye biashara zao, bali katika familia na jamii zao,” amesema Bi. Kambewe.
Nao, washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru FCC kwa kuwaelimisha katika kuhakikisha wanafikia malengo, huku wakieleza kuwa elimu hiyo inakwenda kuwa msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Katika mafunzo hayo, washiriki walipata uelewa kuhusu vitendo vya kibiashara visivyokubalika kisheria nchini Tanzania, vikiwemo upangaji wa bei, kususia kwa pamoja, kupunguza uzalishaji kwa makusudi, upangaji wa zabuni kwa udanganyifu, na mgawanyo wa masoko.
Vilevile, wamejifunza namna ya kutambua bidhaa bandia na kujiepusha na ukiukaji wa sheria za ushindani, ambao zinaweza kuathiri vibaya ukuaji na uendelevu wa biashara zao.
Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za pamoja kati ya FCC na TWCC katika kuwawezesha wajasiriamali wanawake kwa kuwapatia maarifa yatakayowasaidia kuendesha biashara kwa ufanisi katika mazingira yenye ushindani mkubwa.