Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mbuga, Bumbuli – Diwani wa Kata ya Mbuga katika Halmashauri ya Bumbuli, Mheshimiwa Dhahabu Jumaah, amesema bajeti ya Wizara ya Fedha iliyowasilishwa bungeni ni bajeti shirikishi na yenye kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi, hasa waliopo vijijini.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo bungeni, Mheshimiwa Jumaah alisema kuwa bajeti hiyo inalenga moja kwa moja katika kuboresha huduma muhimu za kijamii ambazo zimekuwa changamoto kwa wananchi wa kawaida.
“Sisi tunaangalia mahitaji muhimu kwa wananchi wetu vijijini, na bajeti hii imegusa maeneo yote ya msingi – elimu, afya, maji na umeme,” alisema Mh. Jumaah.
Mheshimiwa Jumaah alisema kuwa bajeti hiyo imeweka msisitizo mkubwa kwenye sekta ya elimu, hususan kwenye miundombinu kama vile madarasa, mabweni na vifaa vya kufundishia. Aidha, upande wa afya pia umepata msukumo mkubwa wa kibajeti, jambo linaloashiria dhamira ya dhati ya serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wote.
“Hii bajeti inakwenda kutatua matatizo ya wananchi wetu – shule zinaimarishwa, zahanati zinapanuliwa na vifaa tiba vinaongezwa. Hii ni hatua kubwa,” aliongeza.
Katika sekta ya maji, diwani huyo alibainisha kuwa serikali imeonyesha dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kupeleka miradi mingi ya maji vijijini. Alisema miradi hiyo inalenga kupunguza adha ya kina mama kutembea umbali mrefu kutafuta maji safi na salama.
“Serikali imewekeza kwenye miradi mikubwa ya maji. Hii ni faraja kubwa kwetu ambao tunaishi vijijini,” alisema.
Kadhalika, sekta ya umeme imepiga hatua kubwa, ambapo kwa mujibu wa Mheshimiwa Jumaah, vijiji vyote katika Halmashauri ya Bumbuli vimefikishiwa umeme, jambo linalowawezesha wananchi kufanya shughuli za maendeleo kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Jumaah alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia vyema utekelezaji wa bajeti za serikali tangu aingie madarakani. Alisema bajeti nyingi zimefikiwa kwa kiwango cha asilimia 100 na hakuna wakati ambapo miradi ya maendeleo imesimama.
“Ukiangalia jengo la Halmashauri ya Bumbuli ni la kisasa kabisa. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais. Bajeti hii pia inaonesha mafanikio makubwa ambayo Taifa limeyapata,” alisema.
Kwa ujumla, bajeti hii inaonekana kuungwa mkono na viongozi wa ngazi ya kata hadi taifa, kwa sababu imeweka mbele maslahi ya wananchi, hasa waishio maeneo ya pembezoni. Ushirikiano kati ya wananchi na serikali ndio msingi wa mafanikio haya.