Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aisha Ally Said akimwelekeza namna ambavyo mishipa ya damu ya moyo inavyoweza kuziba Mpiga Picha Mwandamizi wa magazeti Deus Mhagale alipotembelea banda la taasisi hiyo hivi karibuni kwa ajili ya kupata huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo zilizokuwa zinatolewa katika viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.
………….
Na Shose Romwald – JKCI
13/06/2025 Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) watashiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Angela Muhozya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo yatakayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma tarehe 16 hadi 26 mwezi huu.
Dkt. Angela alisemma huduma hiyo itatolewa bila malipo yoyote ambapo wananchi watapata huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.
“Tutatoa huduma za ushauri wa kiafya kuhusiana na magonjwa ya moyo, elimu ya lishe bora, elimu ya upasuaji wa moyo, elimu ya upandikizaji wa vifaa visaidizi vya moyo, elimu ya uzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo na huduma ya Utumishi na Utawala”.
“Wagonjwa watakaogundulika kuwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu hapo hapo na wale watakaokutwa na matatizo yatakayohitaji matibabu ya kibingwa watapewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam”, alisema Dkt. Angela.
Dkt. Angela alisema kupitia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema; “Himiza matumizi ya mifumo ya kidigitali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji”, wataonesha wananchi namna ambavyo wanatumia mifumo ya kidigitali katika kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo ndani na nje ya nchi.
“Ninawaomba wananchi wa mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani mtembelee katika banda letu na kupima afya zenu kwa kufanya hivi mtaweza kujua kama mna matatizo ya moyo na hivyo kuanza matibabu mapema kwa atakayegundulika kuwa mgonjwa”.
“Pia ukifika katika banda letu utafahamu namna ambavyo Taasisi yetu inavyotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ya mwaka 2015, kupitia Tangazo la Serikali Na. 454 la mwaka 2015”, alisema Dkt. Angela.