Na WMJJWM-New York
Tanzania imeunga mkono Azimio la Umoja wa Mataifa Namba A/79/L.92 la kutambua Juni 27 kuwa Siku ya Kimataifa ya Viziwi Wasioona.
Akizungumza katika Mkutano wa pembeni uliofanyika tarehe 12 Juni, 2025 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju ambaye ni Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu (CoSP 18) amesema Tanzania inatoa shukrani kwa ujumbe wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa wa Kroatia na wadhamini wenza wote kwa kushirikiana na Tanzania kuibua suala hilo muhimu mbele ya ulimwengu, kwakuwa kutambulika kwa siku hiyo kutatoa fursa ya kukuza uelewa wa kimataifa juu ya changamoto za kipekee zinazowakabili viziwi wasioona.
Amesema kuimarisha kutambuliwa kwao ndani ya harakati ya haki za watu wenye ulemavu kutachochea juhudi thabiti za kimataifa kuelekea ujumuishwaji wao, uwezeshaji na ufikikaji wa huduma na fursa kwa usawa kama ilivyo kwa watu wengine.
Aidha, Wakili Mpanju amesema kuadhimishwa kwa siku hiyo kutaimarisha juhudi za kitaifa, kikanda na kimataifa za kuandaa wataalam kama vile watafsiri wa lugha mguso, waelimishaji, na watoa huduma za afya wanaoweza kuwahudumia kwa ufasaha watu wanaoishi na ulemavu mchanganyiko wa macho na usikivu. Hali itakayoboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa kundi hilo kwa kutumia nyenzo na njia sahihi na rafiki za mawasiliano.
Naye Mjumbe wa Kamati Tendaji kutoka Shirikisho la Viziwi wasioona Duniani Christopher Woodfill amesema jamii hii ya viziwi wasioona inahesabika kama watu wenye ulemavu mchanganyiko wapo kwenye kundi la wasioona na pia viziwi. Aina hii ya ulemavu wa uziwi na kutoona au uoni hafifu imesahaulika na kuachwa nyuma karibia kwenye nyanja zote za kimaisha.
Kuadhimishwa kwa Siku hii kutahamasisha Serikali na wadau kukusanya takwimu sahihi na maalum zinazoonesha idadi halisi ya Viziwi wasioona. Takwimu hizo zitakuwa nyenzo muhimu katika utungaji wa sera jumuishi na halisia zikibainisha afua mahsusi za kukabiliana na changamoto na kuweka mifumo wezeshi ya upatikanaji wa mahitaji ya kipekee ya kundi hilo.
Tarehe 16 Juni, 2025 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jijini Newyork litapiga kura kuifanya tarehe 27 Juni kuwa Siku ya Kimataifa ya Viziwi Wasioona.