Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amechangia kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule ya sekondari ya Wasichana ya Ruvu iliyopo Kibaha vijijini mkoani Pwani.
Akizungumza wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia katika Harambee hiyo ambayo ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 510 kati ya shilingi milioni 700 zinazohitajika , Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia anaunga mkono uamuzi huo wenye nia ya kuwafanya wanafunzi katika shule hiyo kusoma katika mazingira salama.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa halmashauri nchini kuendelea kutenga fedha kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa shule katika maeneo hayo badala ya kusubiri Serikali kuu pekee.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Ujenzi ambaye pia ni Katibu wa Itikadi, Uenezi, na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) CPA Amos Makala amesema lengo la kukusanya fedha hizo ni kuhakikisha wanajenga uzio huo ili kuwapa usalama watoto wa kike wanaosoma katika shule hiyo
Harambee hiyo imefanyika jana Jumamosi (Juni 14, 2025) jijini Dar es Salaam.