Na John Bukuku, Dar es Salaam
Katika juhudi za kuboresha elimu nchini, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kuweka msukumo katika kuinua ubora wa walimu kupitia mashindano ya kitaaluma yanayolenga kuongeza ufanisi katika ufundishaji.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa mashindano ya stadi za ufundishaji yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda alisema kuwa Serikali inatambua mchango wa walimu na imepanga kuyaingiza mashindano hayo kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kama njia ya kuongeza motisha kwa walimu.
“Mashindano haya si tu yanatambua ubunifu wa walimu, bali yanahamasisha kubadilishana maarifa na mbinu bora za kufundisha. Ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuboresha elimu kwa vitendo,” alisema Prof. Mkenda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, alisema mashindano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mtaala mpya wa mwaka 2023, ambapo msisitizo mkubwa umewekwa katika matumizi ya TEHAMA na mbinu shirikishi.
“Kwa mwaka huu, tumewashirikisha walimu wa sayansi wa sekondari kwa mara ya kwanza. Hii inaonyesha jinsi gani mashindano haya yanavyozidi kukua na kujumuisha walimu wa ngazi mbalimbali,” alisema Dkt. Komba.
Aidha, alibainisha changamoto ya baadhi ya walimu kurekodi maudhui yasiyofaa na kusisitiza kuwa hilo ni eneo linalohitaji kushughulikiwa ili kuimarisha ubora wa mashindano yajayo.
Naye mwakilishi mkazi wa Benki ya Dunia, Gema John, alieleza kuwa benki hiyo imekuwa mshirika muhimu katika kuinua sekta ya elimu, hasa kwa kuwekeza kwa walimu wa awali, msingi na sasa sekondari.
“Walimu ndio msingi wa elimu bora. Ndiyo maana Benki ya Dunia imeamua kushirikiana na TET kuhakikisha walimu wanapata fursa ya kuonyesha ubora wao na kupata mafunzo ya kuboresha mbinu zao za kufundisha,” alisema Gema.
Mashindano hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa walimu kubadilishana uzoefu na kuhamasisha ubunifu katika ufundishaji, jambo linalosaidia kuandaa wanafunzi bora kwa mahitaji ya sasa na baadae.