Na Mwandishi wetu, Simanjiro
TAASISI ya Chanzo cha Matumaini Tanzania (CHAMATA) na wakazi wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameungana kuadhimisha siku ya akina baba duniani kupitia kauli mbiu ya alipo mama aliyefanikiwa yupo baba aliyesimama kwenye nafasi yake.
Katibu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Chanzo cha Matumaini Tanzania (CHAMATA) Mkoa wa Manyara, Anthony Jacob Mavili amesema maadhimisho ya siku ya akina baba duniani ambapo katika wilaya ya Simanjiro yamefanyika mji mdogo wa Mirerani.
Mavili amesema CHAMATA wametoa kauli mbiu ya siku ya wakina baba duniani kwa mwaka 2025 kuwa ni popote alipo mama aliyefanikiwa, yupo baba aliyesimama kwenye nafasi yake.
Mavili amesema CHAMATA ni taasisi isiyo ya kiserikali yenye kufanya kazi za kisiasa na kijamii ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuyasemea yale yote anayofanya katika maendeleo ya nchi.
“CHAMATA imekuwa na harakati mbalimbali za kumuunga mkono Rais Samia na kuwepo kila mahali ambapo anafanya ziara, kuzindua miradi na mikutano mbalimbali,” amesema Mavili.
Afisa Tarafa ya Moipo, Dhulfa Laizer ambaye alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo ya siku ya wakina baba duniani kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Fakii Raphael Lulandala ameisihi jamii kutoshiriki kusambaza mitandaoni taarifa za kuwakashifu viongozi wa kitaifa.
Laizer amewapongeza CHAMATA kwa kuandaa maadhimisho hayo huku wakizungumza mambo mazuri yaliyofanyika kwenye uongozi wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“CHAMATA mmefanya jambo jema katika maadhimisho haya kwani mmetabeba na pia kutoa ujumbe wa maendeleo mbalimbali yaliyofanyika kupitia Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Laizer.
Diwani wa kata ya Endiamtu, Lucas Zacharia amesema wakati huu anamalizia kipindi chake cha miaka mitano ya 2020/2025 anafurahia miradi mingi ya maendeleo iliyofanyika.
“Pamoja na kuboreshwa na kuanzishwa miradi mingi ya sekta ya afya, elimu na maji, tunajivunia uanzishwaji wa kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Mirerani B.W. Mkapa na kujengwa kwa soko la mnada wa madini ya vito wa Tanzanite city,” amesema Zacharia.
Diwani wa kata ya Mirerani Salome Mnyawi amesema katika kipindi chake cha miaka mitano miradi mingi ya maendeleo imefanyika hivyo anaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Tumefanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kituo kipya cha afya cha Tanzanite, madarasa mapya ya shule na bweni la watoto wenye mahitaji maalum.
Mratibu wa CHAMATA kanda ya kaskazini, Fatuma Kifunta amesema CHAMATA imekuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Tunaomba CHAMATA tuendelee kupewa ushirikiano kwa kupatiwa majukwaa ili tuweze kumsemea vyema Rais Samia Suluhu Hassan kwani amefanya mengi na anastahili miaka mitano tena,” amesema Kifunta.



