Mwamvua Mwinyi, KIBAHA
Juni 16, 2025
Taasisi ya fedha inayojishughulisha na umiliki wa nyumba kupitia mfumo wa mikopo (TMRC), imetoa msaada wa shilingi milioni kumi kwa ajili ya kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili Shule ya Sekondari Mwanalugali, iliyopo Kata ya Mwanalugali, Kibaha mkoani Pwani.
Sehemu ya msaada huo utatumika kupunguza changamoto ya ukosefu wa viti na meza katika bwalo la chakula shuleni hapo.
Ujio wa TMRC umefanikiwa kupitia jitihada za mdau wa maendeleo wa kata hiyo, Dkt. Charles Mwamwaja, ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya elimu katika shule hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya msaada huo katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya, alisema taasisi yake imetoa milioni kumi kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya elimu hivyo shule itaamua kipaumbele kutokana na changamoto zilizopo.
Mgaya aliipongeza serikali ya awamu ya sita kwa juhudi zake za kuboresha mazingira ya elimu na kusisitiza kuwa TMRC itaendelea kushirikiana na serikali katika kuchangia maendeleo ya elimu, ili kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira rafiki.
Nae Dkt. Charles Mwamwaja alisema yeye ni mkazi wa Mwanalugali, hivyo anaguswa moja kwa moja na changamoto za kijamii, ikiwemo mazingira duni ya elimu.
Aidha, alieleza mradi wa Safari Yangu Kwanza (SYK) utazinduliwa hivi karibuni katika shule hiyo, mradi ambao utawajengea wanafunzi uwezo wa kujiamini.
“Mradi huu unawaleta pamoja wataalamu mbalimbali, viongozi, watu maarufu—wanawake na wanaume—ili kuwaeleza wanafunzi safari yao ya maisha na kielimu hadi kufikia walipo sasa,” alieleza Dkt. Mwamwaja.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwanalugali, Uyeka Kessy, alitoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo, ikiwemo ukosefu wa uzio.
Kessy alieleza kuwa ,ukosefu wa uzio umekuwa changamoto kubwa, hasa katika kukabiliana na tabia ya baadhi ya wanafunzi kutoroka shule.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Mwanalugali, Alex Lubawa, aliishukuru serikali kwa kushirikiana na taasisi na mashirika binafsi, na kutoa shukrani kwa TMRC kwa msaada huo wa fedha