
NA DENIS MLOWE IRINGA
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MCC) Salim Abri (Asas) amewataka watia nia wote kuacha matamshi ya kumponda au kuongea yasiyoyofaa kwa chama au kwa kiongozi anayemaliza muda wake badala yake wazungumze kuhusu malengo yao ya kugombea nafasi wanayoomba.
Akizungumza na wanahabari katika ofisi za Ccm Mcc Asas alisema kuwa watia nia hao kujieleza kwa hoja na kueleza mipango yao badala ya kutumia fursa hiyo kuwajadili wagombea wengine waliokuwa madarakani kitu ambacho hakipendezi.
Alisema kuwa katika kipindi hiki kutakuwa na watia nia wengi sana ambao wataita waandishi wa habari na kufanya press hiwatumie vyombo vya habari kutangaza malengo yao ya kuwania uongozi wanaotaka kwani haipendezi kwa watia nia hao kutumia fursa hiyo kuwachafua, kuwakejeli, kuwatukana na kuwashambulia wanachama wenzao.
Aliongeza kwamba Ccm kina taratibu, kanuni na miongozo ambayo kila mwanachama anapaswa kuiheshimu na endapo atashindwa kuzingatia akumbuke kuna vikao vya juu na anaweza kupepetwa kama kuchambua mchele.
Aliongeza kuwa nyakati kama hizi chama kimejipanga vyema kuleta wagombea ambao watakuwa na maadili mazuri ndani na nje ya chama ambao watakuwa msaada mkubwa katika kukiletea ushindi wa kishindo Chama cha Mapinduzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yasin, alisisitiza kutangaza nia si kosa, lakini akasema kufanya hivyo kwa matusi au kuanza kampeni za mapema ni ukiukwaji wa kanuni za chama .
Alisisitiza kauli ya Mcc Asas kwa kutoa onyo kwa watia nia dhidi ya kuanza kuzunguka kata au majimbo, akisema huo ni mwanzo wa kampeni kabla ya wakati na kwamba chama hakitasita kuchukua hatua kwa watakaobainika kuvunja taratibu na kuwaondoa.
Alisema kuwa lengo la chama chochote ni kushika dola hivyo wamejipanga vyema kushinda kwa kishindo uchaguzi mkuu na watawaleta wagombea ambao jamii imewataka kuwaongoza.
Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Said Goha alisisitiza kwamba CCM itaendelea kusimamia haki, usawa na nidhamu katika mchakato wake wa ndani, huku wakihimiza wanachama kutanguliza maslahi ya chama na taifa badala ya maslahi binafsi na kwa wale wanaonza kampeni kabla watachukuliwa hatua.