SERIKALI imesisitiza kuwa imejipanga kuhakikisha kuwa wafugaji nchini wanakuwa na uwezo wa kufanya ufugaji wa kisasa wenye tija zaidi na kuachana na mbinu duni kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya nchi.
Hayo yasemwa jana Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti, wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Tatu ya Mifugo ya Nchi Tatu 2025 yaliyofanyika katika Kijiji cha Ubena Zomozi, Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo, ambapo maonesho hayo yamefadhiliwa na Benki ya NMB na kuandaliwa na Kampuni ya Mbogo Ranches, chini ya kaulimbiu: “Kujenga Ushirikiano, Kukuza Kilimo”.
Maonesho hayo yalihudhuriwa na wafugaji kutoka nchi tatu ambazo ni Tanzania, Kenya na Namibia, pamoja na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Isaac Njenga na Kamishna Mkuu wa Namibia, Lebbius Thobias pamoja na waonyeshaji wa vifaa na bidhaa mbalimbali za kilimo kutoka kampuni mbalimbali.
“Asilimia takribani 97 ya ng’ombe nchini ni wa asili, ambao hutoa wastani wa kilo 80 hadi 120 za nyama kwa ng’ombe mmoja, na maziwa ni kati ya lita moja hadi tatu kwa siku kwa kila ng’ombe. Aina hii ya uzalishaji haina tija, ndiyo maana Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali kuleta mapinduzi katika sekta hii,” alisema Mnyeti.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya ya Biashara Benki ya NMB, Msolo Mlozi alisema kuwa hadi sasa benki hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa wafugaji nchini kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo kunenepesha mifugo, kununua chakula bora cha mifugo, kununua aina bora za mifugo na kujenga miundombinu bora ili kuongeza uzalishaji.
“Benki yetu inafahamu changamoto zinazowakumba wafugaji kama vile uhaba wa chakula na maji hasa wakati wa kiangazi, magonjwa ya mifugo, uzalishaji mdogo kutoka kwa mifugo wa asili, na ukosefu wa makazi ya kudumu kwa wafugaji.
Kupitia mikopo tunayotoa, wafugaji wanaweza kukuza au kununua chakula cha mifugo, kuchimba visima vya kudumu na kutatua tatizo la ukosefu wa maji, pia kuhudhuria mafunzo mbalimbali ya kuongeza maarifa,” alisema Mlozi