NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge amempongeza kwa dhati Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha mjini Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa kuweza kuweka mikakati madhubuti katika kubuni vyanzo vipya vya ukusanyaji wa mapato ya ndani ambayo yameweza kuleta mabadiliko chanya katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ya kimaendeleo.
Amesema kwamba Halmashauri ya Kibaha mji imeweza kupiga hatua kubwa hadi kuweza kupandishwa hadhi ya kuwa Manispaa kutokana na juhudi na ushirikiano ambao unafanya na viongozi mbali mbali wakiwemo wakuu wa idara, baraza la madiwani,mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi mtendaji kwa kuweza kushirikiana na viongozi wenzake katika suala zima la kuleta maendeleo katika nyaja mbali mbali.
“Nampongeza sana Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha mjini Dkt. Rogers Shemwelekwa pamoja na timu yake nzima wakiwemo wakuu wa idara, wataaalamu pamoja na baraza la madiwani ambao kwa kweli mimi siwezi kuoana sababu ya kutowapongeza kwa dhati kabisa akiwemo Mbunge pamoja na Mkuu wa Wilaya ambao wameunganisha umoja na ushirikiano katika suala zima la maendeleo bila kusahau juhudi za kupandisha hadhi kuwa Manispaa,”amebainisha Kunenge.
Aidha Kunenge amewataka viongozi wa Halmashauri ya Kibaha mji kuachana na tabia ya kuwa na mivulugano na vurugu ambazo hazina tija na badala yake wahakikishe wahakikishe wanaungana kwa pamoja katika kusikiliza na kushughulikia kero na changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi.