Dar es Salaam, Juni 17, 2025,
Kampuni ya Bakhresa Group (SSB) imetajwa kuwa mfano bora wa mafanikio ya sekta binafsi nchini Tanzania baada ya kutimiza miaka 50 ya uendeshaji wake, ikiwa imetoa ajira zaidi ya 10,000 moja kwa moja na nyingine zisizo za moja kwa moja zaidi ya 150,000.
Tukio hilo la kihistoria limeadhimishwa leo jijini Dar es Salaam kwa uzinduzi rasmi wa chapa ya maadhimisho ya Miaka 50 ya kampuni hiyo, sambamba na bidhaa mpya ya kifurushi cha unga wa ngano.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Suleiman Serera, amesema mafanikio ya Bakhresa Group ni uthibitisho wa nafasi kubwa inayoshikiliwa na sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wa Taifa, hususan katika viwanda, ajira na ushindani wa kikanda.
“Ukuaji endelevu wa taifa letu unahitaji sekta binafsi yenye ubunifu na uwezo wa kuwekeza ndani na nje ya mipaka ya nchi. Bakhresa Group ni mfano hai wa dhamira hiyo,” amesema Serera.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SSB, Ali Mukadam, amesema kampuni hiyo imeendelea kuongeza uwezo wake wa uzalishaji, ikitoka kuzalisha tani 15 za unga wa ngano kwa siku hadi tani 9,000 kwa siku kote barani Afrika.
Aidha, Mukadam amesema hadi sasa kampuni hiyo imeanzisha jumla ya kampuni 15 ndani ya Tanzania na nyingine nane katika nchi mbalimbali za Afrika, na inakadiriwa kuingiza mapato ya zaidi ya trilioni 2.68 kwa mwaka.