JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mtuhumiwa Seven Kipara [38] mkazi wa Ipwizi kwa tuhuma za kupanga njama na wenzake za kumuua mama yao mzazi na kumjeruhi kwa risasi mtoto aitwaye Sinzo Jifwalo mwenye umri wa miaka 4 mkazi wa Kijiji cha Ipwizi.
Ni kwamba mnamo Juni 13, 2025 saa 6:05 usiku huko Kijiji cha ipwizi kilichopo Kata ya Mjele, Wilaya ya Mbeya vijijini, mtoto aitwaye Sinzo Jifwalo mwenye umri wa miaka 4 alijeruhiwa kwa risasi za shot gun katika bega la kushoto na mdomoni na mtuhumiwa Tabi Deus.
Taarifa za awali zinaonesha kuwa mtoto huyo alikuwa amelala chumbani kitanda kimoja na bibi yake mzaa baba aitwaye Kweji Lugembe [75] na ghafla walisikia mlipuko kutoka eneo la dirishani kisha mtoto huyo kukutwa amejeruhiwa.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa tukio hili linahusishwa na imani za kishirikina ambapo Seven Kipara na Jifaru Kipara [Watoto wa Bibi Kweji Lugembe] wanadaiwa kumtuhumu mama yao Kweji Lugembe kuwa mshirikina anayewaua watoto na wadogo zao. Kutokana na imani hiyo, walipanga njama ya mauaji dhidi ya mama yao huyo kwa kuwakodi wauaji kutoka Mkoa wa lindi ambao ni Tabi Deus na Shija kwa makubaliano ya kuwalipa shilingi milioni tano (5,000,000/=).
Juni 8, 2025 Tabi Deus [39] mkazi wa Kilwa Masoko Mkoa wa Lindi na Shija walifika eneo la Mji Mdogo wa Mbalizi ambapo walipokelewa na mwenyeji wao aitwaye Seven Kipara ambaye aliwapeleka kulala kwenye nyumba ya wageni iliyopo Mbalizi hadi Juni 10, 2025 ndipo mwenyeji wao aliwaonyesha mazingira ya nyumbani kwa mama yao Kweji Lugembe.
Juni 13, 2025 saa 6:05 usiku watuhumiwa hao baada ya kujikiridhisha vya kutosha na mazingira ya nyumbani kwa mhanga walienda hadi katika nyumba ya Kweji Lugembe na baada ya kufika mtuhumiwa Tabi Deus alifyatua risasi mbili kupitia dirishani kwa lengo la kumuua Kweji Lugembe lakini risasi hizo zilikosa lengo na badala yake kumjeruhi mtoto Sinzo Jifwalo na kisha watuhumiwa kutokomea.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Tabi Deus na Seven Kipara (Mtoto wa Kweji Lugembe) ambapo Tabi Deus baada ya kupekuliwa alikutwa akiwa na Pistol moja iliyotengenezwa kienyeji isiyo kuwa na namba na risasi mbili za Shot Gun zikiwa ndani ya mkoba mdogo.
Baada ya mahojiano, Juni 15, 2025 saa 1:00 jioni Tabi Deus [39] aliwaongoza Askari Polisi kwenda kuonesha maficho yao ambako inasadikika mtuhumiwa Shija amejificha pamoja na vitu walivyokuwa navyo ambavyo ni silaha na risasi na baada ya kufika eneo hilo lenye korongo na vichaka, ghafla mtuhumiwa alikurupuka na kuanza kukimbia ndipo Askari walifyatua risasi tatu hewani kwa lengo la kumtaka kutii amri halali ya kusimama lakini mtuhumiwa alikaidi amri hiyo ndipo alipigwa risasi moja katika mguu wake wa kulia na kukamatwa na kukimbizwa katika Hospitali Teule ya Ifisi kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini alifariki dunia.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako dhidi ya watuhumiwa wengine waliohusika katika tukio hili.
MWANAFUNZI WA MUST ASHIKILIWA KWA MAUAJI YA MWENZAKE.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya [MUST] mwaka wa kwanza aitwaye Emilian Joseph Duzu [21] kwa tuhuma za mauaji ya Mwanafunzi mwenzake wa Chuo hicho mwaka wa tatu aitwaye Gerald Philbert Said [22].
Ni kwamba Juni 14, 2025 saa 11:00 Alfajiri huko katika Klabu iitwayo Mbeya Pazuri iliyopo Jijini Mbeya mtuhumiwa Emilian Joseph Duzu [21] alimjeruhi Gerald Philbert Said [22] ambaye kwa sasa ni marehemu kwa kumchoma kitu chenye ncha kali tumboni hali iliyopelekea kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu lakini ilipofika saa 7:00 mchana Gerald Philbert Said [22] alifariki dunia.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokana na ulevi wa kupindukia wakiwa eneo la ndani la klabu hiyo ambapo walinzi [Mabaunsa] waliwaamua na ndipo mtuhumiwa alitoka nje na kuelekea eneo la maegesho alipokuwa ameegesha gari ndipo Gerald Philbert Said [22] ambaye kwa sasa ni marehemu alimfuata kwa lengo la kuendelea kugombana ndipo mtuhumiwa alimchoma kwa kitu chenye ncha kali.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja kwani havina nafasi katika jamii na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lipo makini na halitasita kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa Wanafunzi kuzingatia masomo na kujiepusha na vitendo visivyofaa ikiwemo ulevi wa kupindukia kwani ni hatari kwa afya zao na maisha yao.
Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.