Na.Bolgas Odilo _DODONMA
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umesisitiza azma yake ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma ya umeme na matumizi ya nishati safi, huku ukieleza kuwa kazi hiyo inaendelea kwa kasi kutoka vijiji hadi vitongoji vyote nchini.
Akizungumza leo Juni 16, 2025 jijini Dodoma, katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Mkurugenzi wa Utawala wa REA, Renetus Msangira, amesema taasisi hiyo kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi na uongozi mzima wa REA, inatoa shukrani kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kuwaalika kushiriki katika maonesho hayo muhimu.
“Tunawashukuru kwa fursa hii ya kuonesha kazi tunazofanya na kujibu hoja za wananchi,REA imefanikiwa kuweka umeme kwenye vijiji vyote, na sasa tumejielekeza kwenye vitongoji ili kuhakikisha kila kaya inapata huduma hii muhimu,” alisema Msangira.
Ameongeza kuwa lengo kubwa la REA ni kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati salama, endelevu na rafiki kwa mazingira, akieleza kuwa taasisi hiyo imekuwa ikigawa majiko ya gesi yenye kutumia “unit moja kwa saa” kama sehemu ya kampeni ya kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
“Kama mnavyoona, katika banda letu hapa maoneshoni, tunatoa elimu na pia tunaonesha majiko yanayotumia umeme au gesi kwa ufanisi mkubwa. Hili ni mojawapo ya mikakati yetu ya kulinda mazingira na afya za wananchi,” aliongeza.
Katika kuhakikisha taasisi za umma nazo zinaingia kwenye matumizi ya nishati safi, REA tayari imetekeleza mpango wa kusambaza nishati safi kwenye taasisi kama vile magereza, na sasa imejielekeza kwenye taasisi nyingine ikiwemo shule, vituo vya afya na maeneo ya kijamii.
Mkurugenzi huyo pia amewaalika wananchi wote, kutoka ndani na nje ya Dodoma, kufika katika viwanja vya maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ili kujionea huduma zinazotolewa na REA, na kupata nafasi ya kutatua changamoto wanazokumbana nazo kuhusu upatikanaji wa nishati vijijini.
Amesema mafanikio hayo yamewezekana kutokana na ushirikiano mzuri kutoka kwa wadau wa maendeleo wanaosaidia kufanikisha miradi ya usambazaji umeme na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi.
“Tunawashukuru sana wadau wetu kwa sapoti yao ya muda mrefu. Pamoja, tunaamini tunaweza kufanikisha lengo la kuhakikisha kila Mtanzania, hata wa kipato cha chini, anapata nishati bora,” alihitimisha Msangira.