Na. Mwandishi wetu Zanzibar.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limekuwa miongoni mwa wadau wakuu wanaoshiriki kunadi fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Hifadhi za Taifa 21 kwenye Mkutano wa Uwekezaji Zanzibar (Zanzibar Investment Summit 2025), uliofanyika kwa mara ya kwanza Kisiwani Pemba huku ukifunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Mhe. Dkt. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kutumia mkutano huo kama jukwaa la kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo Zanzibar hususan kisiwani Pemba na maeneo mengine ya Tanganyika hasa maeneo ya Hifadhi za Taifa.
Aidha, alitilia mkazo zaidi kwa wawekezaji wa ndani na nje kuchangamkia mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Katika Mkutano huo ulioanza June 15, 2025 TANAPA ilijikita kutangaza fursa za uwekezeji katika mazao ya utalii pamoja na miundombinu ya malazi kwa watalii wanaotembelea vivutio hivyo vilivyosheheni aina mbalimbali ya wanyama, mimea na mandhali za kuvutia zenye uoto wa asili ikijumuisha mabonde, milima na mito.
Mbali na kunadi fursa za uwekezaji pia, Wahifadhi hao walihamasisha watanzania na wawekezaji mbalimbali waliohudhulia mkutano huo kutembelea Hifadha za Taifa mbalimbali kutokana na upekee wa kila hifadhi ili wawe mabalozi wazuri wa kuzinadi hifadhi hizo warudipo nchini kwao na kuongeza kasi ya ujio wa watalii ili kukuza pato la Taifa.
Mkutano huo unaotarajiwa kutamatika leo June 17, 2025 ukibeba kauli mbinu isemayo; “Ni Wakati wa Pemba”pia unawajumuisha wadau kutoka sekta za utalii, kilimo, uchumi wa buluu, miundombinu, na biashara kutoka mataifa mbalimbali.