Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam – Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imepiga hatua kubwa katika mageuzi ya elimu kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Taasisi hiyo imezindua mifumo mipya ya kidijitali inayolenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji nchini.
Maadhimisho hayo yameambatana na uzinduzi wa Soma Kwanza TV, Mfumo wa Ufundishaji na Ujifunzaji wa Walimu (LMS) na Jalada la kitabu cha hadithi cha ‘Bi Mkubwa na Wajukuze’, vyote vikiwa na lengo la kuimarisha ujifunzaji kwa njia bunifu, jumuishi na rahisi kufikiwa na walimu pamoja na wanafunzi kote nchini.
Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliipongeza TET chini ya Mkurugenzi Mkuu wake, Dkt. Aneth Komba, kwa ubunifu na juhudi kubwa katika kuimarisha elimu kwa kutumia teknolojia.
“Leo tunashuhudia mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kupitia mifumo hii mipya. TET haijabaki nyuma, bali inakwenda sambamba na dunia katika kuleta suluhisho la kweli kwa changamoto za ufundishaji,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mifumo hiyo inatumika ipasavyo, hasa kwa kushirikiana na wadau wa mawasiliano kama Airtel na Vodacom ili kuhakikisha upatikanaji nafuu wa huduma za intaneti kwa shule na walimu.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda alisema TET imeweka msisitizo katika matumizi ya njia mbadala za kidijitali kufundishia, sambamba na kuendeleza uandishi bunifu wa vitabu, riwaya na tamthiliya.
“Tumeanzisha Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ili kuhamasisha Watanzania kuandika vitabu vya kiwango cha juu vitakavyotumika katika mfumo rasmi wa elimu,” alisema Prof. Mkenda.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba alisema uzinduzi wa Soma Kwanza TV unalenga kurusha maudhui ya kielimu kwa saa 24, kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu. Alisema chaneli hiyo kwa sasa inapatikana kupitia Startimes namba 105 na kuna mipango ya kuipeleka kwenye ving’amuzi vyote na hata kuzindua TET Soma Kwanza Radio.
“Tunaamini elimu ni haki ya kila mtoto, na teknolojia ndiyo daraja la kuifikia jamii kwa upana wake,” alisema Dkt. Komba.
Kwa kauli mbiu ya mwaka huu “Kitabu Kimoja kwa Mwanafunzi Mmoja”, TET imedhihirisha kuwa mageuzi ya elimu si ndoto, bali mchakato unaoendelea kujengwa kwa bidii, ubunifu na ushirikiano wa kweli kati ya serikali na wadau.