Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Balozi wa Italia nchini Tanzania Mhe. Giuseppe Coppola katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam wakati Makamu wa Rais akielekea Jijini Roma nchini Italia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Ubia wa Maendeleo kati ya Afrika na Serikali ya Italia (Mattei Plan). Tarehe 18 Juni 2025.
…….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango, leo tarehe18 Juni 2025 ameondoka nchini kuelekea Italia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Ubia wa Maendeleo kati ya Afrika na Serikali ya Italia (Mattei Plan) pamoja na Mpango wa Umoja wa Ulaya (EU Global Gateway) utakaofanyika Jijini Roma, tarehe 20 Juni 2025.Mkutano huo unatoa fursa kwa Tanzania kunufaika na mipango mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na nchi ya Italia (kupitia Mattei Plan) na Umoja wa Ulaya (kupitia EU Global Gateway).
EU Global Gateway ni mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuboresha miundombinu katika sekta za kidijitali, nishati, usafirishaji, afya, elimu, na utafiti. Mpango huu unalenga uwekezaji wa Euro bilioni 300 ifikapo mwaka 2027, ambapo Euro bilioni 150 zimeelekezwa barani Afrika. Aidha, Makamu wa Rais anatarajiwa kushiriki katika Mikutano ya Uwili yenye lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania, Mataifa na Mashirika yanayoshiriki Mkutano huo.