Wakili wa Serikali, Grace Thadei Komba, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kufika katika viwanja vya Maturubai, Mbagala Kizuiani, Wilaya ya Temeke, ili kupata msaada wa kisheria kabla ya muda wa kampeni hiyo kufikia kikomo.
Akizungumza na Full Shangwe leo, Komba alisema kuwa mwitikio wa wananchi katika kampeni ya Mama Samia Legal Aid Campaign ni mzuri, lakini amesisitiza umuhimu wa wale ambao bado hawajafika kuchangamkia fursa hiyo ya bure.
“Mwitikio ni mzuri ila naendelea kuwahimiza walewote wenye matatizo ya kisheria ambao bado hawajafika hapa wafike mapema maana siku zimebakia chache. Waje wahudumiwe na timu kubwa ya wanasheria, ambapo ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko tayari kuwahudumia,” alisema Komba.
Aliongeza kuwa kampeni hiyo, inayoendeshwa na Wizara ya Katiba na Sheria, itaendelea hadi Juni 27, 2025, na imekusudia kutoa huduma kwa wananchi wa kawaida wasioweza kumudu gharama za kisheria.
Baadhi ya wananchi waliopata huduma hiyo leo wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuanzisha kampeni hiyo ya msaada wa kisheria, wakieleza kuwa imewasaidia kupata haki zao bila gharama.
“Kwanza kabisa namshukuru sana Rais Samia. Mimi ni mwananchi wa kawaida tu, siwezi kumudu gharama za kumlipa wakili, lakini nimefika hapa, nimepokelewa vizuri na nimepewa muda wa kusikilizwa. Naondoka nikiwa na matumaini kwamba jambo langu linashughulikiwa kisheria na haki itatendeka,” alisema Adolf Shirima, mmoja wa wananchi waliopata msaada huo.
Kampeni hii inalenga kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi kupitia huduma rafiki na jumuishi, huku ikisisitiza usawa mbele ya sheria kwa wote.