Chama Kikuu cha Wakulima wa Mara (Wamacu) kwa kushirikiana na wadau wa zao la tumbaku wanatarajia kuongeza uzalishaji wa zao hilo mkoani Mara kutoka tani 2,600 hadi tani 5,000 katika msimu wa kilimo wa 2025/26.
Matarajio hayo ni baada ya kubaini changamoto zinazokabili uzalishaji wa zao hilo ambapo wadau hao kwa pamoja wameweka mikakati ya namna ya kumaliza changamoto hizo ili wakulima waweze kufanya shughuli zao katika mazingira rafiki.
Akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa wadau kujadili maendeleo ya zao hilo mjini Mugumu leo Juni 18,2025, Meneja Mkuu wa Wamacu, Samwel Gisiboye amesema wamebaini wakulima wa zao hilo walikuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi zilizokuwa zinasababisha uzalishaji wa zao hilo kuwa wa chini.
Amesema sababu hizo ni pamoja na kuchelewa kwa pembejeo na mbegu hali ambayo kwa namna moja ama nyingine ilikuwa ilisababisha zao hilo kutostawi na kutoa mazao kama ilivyotarajiwa.
“Tunajua kuwa wakati wa kupanda mkulima anatakiwa kuwa na mbegu na pembejeo ili akipanda tu anaweka mbolea na baada ya muda anatakiwa kupulizia dawa lakini wakulima wa hapa walikuwa wanapokea mbegu kwanza na wakishapanda wanaanza kusubiri pembejeo jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa ustawi wa tumbaku,” amesema
Amesema suala lingine ni kuchelewa kwa msimu wa mauzo ya tumbaku ikilinganishwa na nchi jirani ya Kenya ambapo msimu wao wa mauzo huanza Desemba huku msimu mauzo kwa wakulima wa Mara ukianza Januari.
Amesema changomoto hizo pamoja na mambo mengine zimesababisha wakulima kufanya shughuli zao bila tija huku wengine wakilazimika kutorosha tumbaku na kwenda kuuza nchini Kenya kwa lengo la kujipatia kipato.
“Uzalishaji usio kuwa na tija umesababisha hadi wakulima kukwepa kulipa mikopo, hivi sasa wakulima wanadaiwa mamilioni ya pesa na taasisi za fedha hii imeleta migogoro kati ya taasisi hizi na wakulima,kwahiyo msimu huu tunahakikisha haya mambo hayatakuwepo isipokuwa tunakuwa na uzalishaji wenye manufaa,” amesema
Baadhi ya wakulima wa tumbaku wamesema endapo changamoto hizo zitapata utatuzi wa kudumu zao la tumbaku linaweza kuwa miongoni mwa mazao makuu ya biashara mkoani Mara.
Rhobi Adam amesema umefika muda mamlaka husika zinatakiwa kuiga mfano wa nchi jirani ya Kenya ambapo maandalizi ya msimu haunza mapema ambapo wakulima wanakuwa na uhakika wa kupata pembejeo na mbegu kwa wakati.
Amesema mazingira bora ya kilimo cha zao hilo yatasaidia uwepo wa kilimo chenye tija hivyo kusaidia kuinua hali ya uchumi wa wakulima na jamii kwa ujumla.
“Hili zao likisimamiwa vizuri litakuwa mkombozi kwa wakulima kwani litakuwa zao kuu la biashara na kwa mujibu wa hali ya soko, zao la tumbaku linalipa sana kinachotakiwa ni kuwa na utaratibu mzuri kuhusu kilimo chake,wakulima sisi tuko tayari,” amesema Chacha Nchagwa
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dk Halfan Haule amesema upatikanaji wa pembejeo kwa wakati ni changamoto kubwa inayokwamisha uzalishaji wa zao hilo hivyo kuziagiza mamlaka husika kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi wa haraka kabla kuanza kwa msimu wa kilimo Julai Mosi mwaka huu.
“Kilimo cha tumbaku kikifanyika kisasa na kuhakikisha kila kitu kinapatikana kwa wakati hakika uchumi wa wakulima utaimarika mara tatu zaidi ya sasa, hivi vikwazo vilivyotajwa vipatiwe ufumbuzi haraka sana,tunataka kuondoa umasikini katika jamii na kilimo hiki ni moja ya mkakati wa kuondoa umasikini,” amesema Dk Haule
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele ameziomba taasisi za fedha kutoa mikopo kwa wakati kwa wakulima hao huku akiziomba kungalia namna ya kupunguza riba ili mikopo hiyo iweze kuwanufaisha wakulima na jamii.
Meja Gowele amesema kilimo cha tumbaku kina mchango mkubwa katika mapato ya halmashauri na wananchi hivyo wadau wanapaswa kushirikiana ili kiwe chenye tija zaidi.
Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Mara,Lucas Kihondere amesema baada ya kubaini changamoto zinazowakabili wakulima wa zao la tumbaku,waliamua kukabidhi sekta hiyo kwa Wamacu ikiwa ni njia mojawapo ya kupambana na changamoto hizo na kufanya kilimo hicho kuwa na manufaa kwa wakulima na jamii.
Amesema awali wakulima walikuwa wakizalisha tani 700 kwa msimu mwaka 2023/24 lakini baada ya Wamacu kuanza kusimamia zao hilo uzalishaji huo umepanda hadi kufikia tani 2,600 kwa msimu wa 2023/25 hivyo upo uwezekano mkubwa wa uzalishaji huo kuongezeka hadi kugika tani 5,000 kwa msimu ujao kama ilivyokusudiwa.
“Tunataka kuanzisha ushirika katika kila sekta na mafanikio kama haya ya kwenye tumbaku yatasaidia kufanikisha malengo yetu kwani tunataka kuwa na ushirika kwenye kila sekta ikiwepo madini, mifugo, uvuvi na kwingineko jwani tunaamini ushirika ni biashara na ushirika ni uchumi,” amesema
Mkuu wa Idara ya Kilimo wilayani Serengeti, Bwenda Bainga amesema tayari mamlaka husika kwa kushirikiana na wadau wameanza kushughulikia changamoto hizo ili kuwasaidia wakulima wafanye shughuli zao bila kikwazo.
“Tumefanya sensa ya wakulima na kupata mahitaji yao halisi ya pembejeo na mahitaji mengine muhimu na hii ni katika maandalizi ya kuanza kwa msimu hivyo mchakato tayari umeanza wa kuagiza mahitaji hayo tunataka msimu ukianza pasiwepo changamoto ya aina yoyote,” amesema