Na John Mapepele OR- TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe Mohamed Mchengerwa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi trioni sita kwa ajili ya huduma mbalimbali ili kuboresha maisha wananchi.
Mhe. Mchengerwa ametoa shukrani hizo leo Juni 18, 2025 kwenye mkutano wa majumuisho ya ziara ya kikazi ya Rais Samia Suluhu Hassan kukagua utekelezaji wa mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wa Simiyu kabla ya kumkaribisha Mhe. Rais kuongea na maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Leo ilikuwa siku yake ya nne baada ya kukagua miradi katika wilaya za Bariadi, Meatu, Itilima na Maswa.
Akitoa maelezo ya awali ya sekta za elimu, afya na miundombinu Mhe. Mchengerwa amemshukuru Rais kwa kutoa fedha nyingi katika sekta hizo katika kipindi kifupi cha uongozi wake.
“Mheshimiwa Rais naomba kusema kuwa wananchi kubwa na wewe kutokana na kazi kubwa uliyoifanya, uongozi wako umejenga imani kubwa na alama isiyofutika vizazi hata vuzazi”. Amefafanua Waziri Mchengerwa
Aidha, amesema baba wa taifa letu Mwalimu Nyerere amesisitiza kuwa maendeleo ni watu dhana ambayo Mhe. Rais Samia ameiendeleza vema.
Akizungumzia eneo la afya amesema Serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali katika mikoa yote kwa gharama kubwa huku akitolea mfano wa Mkoa wa Simiyu kuwa ulipatiwa jumla ya shilingi bilioni 46.7 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na vifaa tiba katika kipindi hiki na kutaja baadhi ya vitu kuwa ni ujenzi wa Hospitali 6 vituo vya afya 16 na magari ya kubebea wagonjwa 14.
Kwa upande wa elimu amesema Serikali imekuwa ikitoa takriban shilingi bilioni 40 kila mwezi ambapo Mkoa wa Simiyu umeshapatiwa shilingi bilioni 28.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule 41 na madarasa 634.
Pia amesema Mkoa wa Simiyu umeshapatiwa shilingi bilioni 14.1 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya utawala ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Ameongeza kuwa shilingi bilioni 3.9 zilitolewa kwa ajili ya kuviwezesha vikundi mbalimbali 420.
Kuhusu ujenzi wa barabara amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 72.489 kwa ajili ya kujenga mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 4163.
Aidha Waziri Mchengerwa amesema tayari Mhe. Rais ameelekeza kujengwa kwa soko la kisasa mjini Bariadi kupitia mradi wa kukuza miji chini ya TAMISEMI ambalo litagharimu shilingi bilioni 26 pamoja na kipande cha barabara chenye kilomita 8.6 ambapo mkataba baina ya mkandarasi na Serikali utasainiwa Juni 25, mwaka huu.
Mhe. Rais Samia pia ameelekeza barabara za ndani zitengenezwe pamoja na kuweka taa ili wafanyabiashara waweze kufanya biashara kipindi chote.
Kwa upande wa mikopo, Mhe. Rais amewataka watendaji kulegeza masharti ya ukopaji ili wananchi waweze kukopa.