Na Mwandishi wetu, Mirerani
DIWANI wa Kata ya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Salome Nelson Mnyawi amempongeza mdau wa maendeleo wa mkoa huo Taiko Kulunju Ole tipa kwa kusimamia vyema ujenzi wa kituo kipya cha afya cha Tanzanite cha kata hiyo.
Diwani Salome ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya wakina baba duniani ambapo kiwilaya imefanyika mji mdogo wa Mirerani na kuratibiwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Chanzo cha Matumaini Tanzania (CHAMATA).
Amesema kwa wakati huu anapomalizia kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano ya 2020/2025 hata sita kutoa pongezi kwa mdau wa maendeleo Taiko Kulunju na wajumbe wa kamati ya ujenzi wa kituo hicho cha afya.
“Mdau wa maendeleo Taiko Kulunju, mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mirerani Namnyaki Lukumay na wajumbe wa kamati ya ujenzi wanastahili pongezi kubwa kwa usimamizi wa ujenzi huo,” amesema Salome.
Amesema Taiko Kukunju na wajumbe hao wamesimamia ujenzi wa kituo kipya cha afya cha Tanzanite cha kata ya Mirerani kwa kumetumia gharama za shilingi milioni 500 zilizotolewa na Serikali.
“Pamoja na pongezi hizo kwa Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi Taiko Kulunju na wajumbe wake naishukuru Serikali kwa kutuongezea shilingi milioni 50 za kukamilika kituo hicho cha afya,” amesema Diwani Salome.