KAMPUNI ya Dough Works Limited (DWL) imezindua rasmi mgahawa mpya wa KFC katika kituo cha mafuta cha TotalEnergies kilichopo Ubungo, Shekilango, jijini Dar es Salaam. Huu ni mgahawa wa 12 wa KFC nchini Tanzania, hatua inayoonesha kasi ya ukuaji wa chapa hiyo pamoja na dhamira ya kutoa huduma bora kwa Watanzania.
Mgahawa huu umejengwa katika eneo la kimkakati lenye shughuli nyingi za kibiashara na makazi, kwa lengo la kuwapatia wakazi wa Ubungo na maeneo jirani chakula bora katika mazingira ya kisasa yanayoendana na viwango vya kimataifa. Wateja watafurahia urahisi wa kupata vyakula vyao pendwa wakiwa karibu na huduma za mafuta na rejareja.
Katika kuonyesha kuthamini uaminifu wa wateja wake, baadhi ya wateja waaminifu walipewa fursa ya kuonja huduma na mazingira ya mgahawa huo kabla ya kufunguliwa rasmi.
Akizungumza leo Juni 19, 2025 katika hafla ya uzinduzi, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mheshimiwa Albert Msando, amesema kwamba ushirikiano kati ya KFC na TotalEnergies ni sehemu ya mkakati wa DWL wa kupanua huduma zake nchini kwa kushirikiana na wadau wanaojali ubora, huduma na ubunifu.
“Ushirikiano huu unaleta suluhisho la huduma kwa wateja – kuanzia mafuta ya magari hadi chakula kitamu katika sehemu moja.” alisisitiza Msando.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa DWL, Bw. Vikram Desai, amesema kuwa mgahawa huu mpya umeunganishwa na teknolojia ya kisasa kama vile self-service kiosks ili kurahisisha mchakato wa kuagiza chakula na kupunguza foleni.
“Huu si uzinduzi wa mgahawa tu, bali pia ni uwekezaji katika jamii kwa njia ya ajira, msaada wa kijamii na utoaji wa huduma za kiwango cha juu kwa Watanzania,” amesema Desai.
DWL kwa sasa inaajiri zaidi ya wafanyakazi 800 kupitia migahawa yake ya KFC, Pizza Hut na BAO Café, ikijipambanua kama moja ya kampuni zinazokua kwa kasi katika sekta ya huduma za chakula nchini. Kila mgahawa mpya huchangia ajira, maendeleo ya ujuzi na uchumi wa ndani. Desai ameongeza:
“Kwa sasa, wakazi wa Ubungo na maeneo ya jirani wanaweza kufurahia ladha ya kipekee ya KFC inayojulikana duniani kwa kauli mbiu ya ‘finger lickin’ good’. Iwe ni wakati wa kujaza mafuta au kutafuta chakula cha haraka, KFC Total Shekilango iko tayari kuwahudumia kwa ladha, urahisi na ubora wa hali ya juu.”
Katika kuadhimisha uzinduzi huu, KFC iliandaa tukio maalum la kijamii kwa kuwaalika watoto kutoka Kituo cha Kulelea Yatima cha Al-Madina kilichopo Tandale kwa Tumbo mnamo tarehe 18 Juni 2025 kwa mlo wa pamoja. Tukio hilo lilijaa vicheko, furaha na mshikamano, likionesha dhamira ya KFC ya kuendelea kuwa karibu na jamii.
Kwa niaba ya Mkurugenzi wa TotalEnergies, Abdu Rahim Saddique amesema kuwa huu ni mgahawa wa pili wa KFC kujengwa ndani ya vituo vya mafuta vya TotalEnergies, baada ya ule wa KFC Magomeni uliotanguliwa kufunguliwa Machi 12, 2024.
“Ujenzi wa mgahawa huu unaonesha maendeleo ya kweli katika ushirikiano wetu na DWL na ni hatua nyingine kuelekea kutoa huduma za kisasa kwa wateja wetu kote nchini,” alisema Saddique.
Ameongeza kuwa KFC Total Shekilango ni ishara ya dhamira ya pamoja kati ya TotalEnergies na DWL katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora zaidi katika maeneo ya kimkakati.

Picha ya pamoja.