Dar es Salaam. Kocha maarufu wa mchezo wa kuogelea duniani, Atiba Wade kutoka Marekani ataendesha mafunzo ya mchezo huo kuanzia Juni 27 mpaka Julai Mosi nchini.
Wade ambaye pia muigizaji wa filamu ataendesha mafunzo hayo kwa kushirikiana na Champion Rise Sports Promoters.
Kocha Wade ameshiriki katika filamu mbalimbali za Hollywood kama Black Panthe, Wakanda Forever (2022), Kaleidoscope (2023), na Pride (2007).
Mkurugenzi wa Champion Rise Sports Promoter Amina Mfaume alisema jana kuwa mbali ya mafunzo ya kuogelea kwa waogeleaji, kocha Wade ataendesha kozi ya Kimataifa ya makocha wa mchezo huo inayotambulika na Chama cha Makocha wa Kuogelea Marekani (ASCA) kuanzia Julai Mosi mpaka Julai 7.
Amina alisema kuwa lengo la kozi hiyo ni kuinua viwango vya makocha wa kuogelea hapa Tanzania.
“Mpango huu utaanza kwa mafunzo ya waogeleaji ambapo wanamichezo chipukizi watafaidika moja kwa moja na ujuzi wa kocha Wade katika kuboresha mbinu za kuongeza.
Baada ya mafunzo ya waogeleaji, itafuata kozi ua makocha ambayo ni fursa ya kipekee kwa makocha,” alisema Amina.
Kuhusiana na kozi ya makocha, Amina alisema kuwa kozi hiyo ni muhimu na inatambulika kimataifa itawezesha makocha wa ndani kujifunza mbinu za kisasa na maarifa yanayolingana na viwango vya kimataifa.
“Mpango huu utatoa maarifa ya kina kuhusu mbinu mbalimbali za mchezo wa kuogelea ikiwa pamoja na mitindo ya kuogelea, falsafa za mazoezi, ukuzaji wa wanamichezo, na saikolojia ya michezo,” alisema.
Alifafanua kuwa kocha Wade ni mtu mashuhuri katika mazoezi ya utendaji wa hali ya juu na mbinu mbalimbali.
Mbali na umahiri wake kama kocha aliyeidhinishwa na ASCA, Wade pia ana uzoefu wa kipekee unaojumuisha michezo na filamu.
Uzoefu wake umemwezesha kufanya kazi na watu mbalimbali maarufu duniani.
Alisema kuwa makocha watakaohudhuria watapata mtazamo wa kipekee wa jinsi ya kuongeza utendaji wa wanamichezo kupitia mbinu mbalimbali za mafunzo.
“Tuna furaha kubwa kuleta kozi ya kuthibitishwa na ASCA na kliniki maalum ya waogeleaji wa kiwango cha juu hapa Tanzania. Hii ni heshima na fursa pekee kwa waogeleaji na makocha kupata mafunzo ya mchezo wa kuogelea kutoka kwa Wade, ” alisema Amina.
Alisema kuwa dhamira ya Champion Rise Sports Promoters ni kuinua mchezo wa kuogelea nchini kwa kiwango juu na ndiyo maana wameamua kuleta kozi hiyo na kocha maarufu.