Na Prisca Libaga Arusha
Nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) zimetakiwa kuongeza kasi ya matumizi ya teknolojia za kisasa na kuwekeza katika bidhaa na huduma bunifu zinazokidhi mahitaji ya soko, ikiwa ni hatua madhubuti ya kuboresha mchango wa sekta ya posta katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika.
Wito huo umetolewa jijini Arusha na Postamasta Mkuu wa Tanzania, Macrice Mbondo, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Utawala la PAPU, unaowakutanisha viongozi wa juu wa taasisi za posta kutoka nchi mbalimbali za Afrika kujadili mustakabali wa huduma za posta katika enzi ya kidijitali.
Mbondo alisema kuna haja ya sekta ya posta barani Afrika kuelekea kwenye mabadiliko ya kidijitali kwa kuunganisha huduma kama vile fedha za kielektroniki, majukwaa ya biashara mtandaoni na mifumo ya ufuatiliaji wa mizigo ili kutoa huduma zenye ushindani wa kimataifa.
“Tunahitaji kuwekeza kwenye miundombinu ya kidijitali na kuleta huduma bunifu zinazolingana na mahitaji ya wateja wa sasa. Taasisi za posta barani Afrika zinapaswa kuwa kitovu cha huduma shirikishi, hasa katika maeneo ambayo mifumo ya jadi ya kifedha na biashara mtandao haijafikia kwa urahisi,” alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa mwelekeo wa dunia kuelekea katika kidijitali unahitaji Afrika kuachana na mifumo ya posta ya kizamani na kuchangia kikamilifu katika mageuzi ya kiuchumi ya bara hili.
Mbondo alibainisha pia changamoto kuu zinazokabili sekta ya posta barani Afrika, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya kidijitali, mwenendo wa watumiaji, ushindani mkali wa kimataifa na mifumo mipya ya biashara.
“Changamoto hizi zinahitaji majibu ya pamoja, bunifu, jumuishi na yanayoongozwa kwa mshikamano wa Kiafrika. Katika muktadha huu, taasisi kama PAPU zinapaswa kuendelea kubadilika, kuvumbua na kuwa vinara katika kuunda mfumo wa baadaye wa huduma za posta barani,” alisema.
Pia alitoa wito kwa wajumbe wa baraza kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma katika kupata huduma bora za mawasiliano na usafirishaji wa bidhaa, bila kujali eneo analotoka.
“Tuna imani kuwa maarifa yenu ya pamoja, uzoefu na maono yenu yatazaa maazimio yatakayochochea ukuaji na mageuzi ya sekta ya posta Afrika — kwa manufaa ya uchumi wetu, taasisi zetu na zaidi ya yote, watu wetu.”
“Kwa upande wa Tanzania, tupo tayari kuendelea kushirikiana nanyi kwa karibu, si tu kama wenyeji wa makao makuu ya PAPU, bali kama washirika wa kweli katika dhamira ya pamoja ya kuendeleza maendeleo ya Afrika.”
Awali, Katibu Mkuu wa PAPU, Sifundo Moyo, alisema mkutano huo umejengwa juu ya misingi ya mikutano iliyopita kwa lengo la kukusanya maoni, mapendekezo na mitazamo ya kuandaa mikakati ya kuboresha utendaji wa taasisi hiyo.
Alieleza kuwa sekta ya posta Afrika kwa sasa inapitia kipindi cha mabadiliko makubwa yanayotokana na maendeleo ya teknolojia, changamoto za kimazingira, na matarajio makubwa kutoka kwa wananchi.
“Wananchi wetu hawategemei tena huduma za kawaida. Wanahitaji huduma zenye mnyumbuliko, upatikanaji rahisi na zinazoaminika,” alisema.
“Wanatarajia huduma zitakazounganisha vijiji na miji, zitakazochanganya masoko rasmi na mitandao ya kimataifa, na zitakazotoa ujumuishaji wa kifedha kwa makundi yasiyohudumiwa ipasavyo.”
“Kwa kuzingatia hali hiyo, hatuwezi kushughulikia changamoto za leo kwa fikra za jana. Ndiyo maana tupo hapa kuchochea ari mpya, kuimarisha mbinu zetu na kuthibitisha tena dhamira yetu ya pamoja,” alihitimisha Moyo.





