Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi, akisalimiana na Afisa Mkuu wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, baada ya kupata maelezo ya elimu ya elimu ya fedha ambayo ni moja ya huduma inayotolewa katika Banda la Wizara ya Fedha, katika Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.
Na. Peter Haule na Saidina Msangi, Dodoma
Afisa Mkuu wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, amewataka wakazi wa Dodoma na maeneo mengine nchini kufahamu gharama za mkopo na kuziafiki kabla ya kuchukua mkopo wowote.
Bw. Kimaro aliyasema hayo wakati akitoa elimu ya fedha kwa watu waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.
Alisema kuwa gharama zinazotakiwa kuangaliwa ni pamoja na riba na ada nyingine zilizoainishwa katika mkataba wa mkopo.
Bw. Kimaro alisema kuwa kabla ya kuchukua mkopo ni vema kumuuliza mkopeshaji kuhusu jumla ya kiasi kinachopaswa kulipwa katika kipindi chote cha mkopo na ni wajibu wa mkopeshaji kumfahamisha mkopaji jumla ya gharama zote zinazohusiana na mkopo husika.
Alisema kuwa riba inaweza kuwa inabadilika au isiyobadilika (Flat interest Rate) ambapo riba inayobadilika hutolewa kulingana na kiasi cha mkopo ambacho hakijarejeshwa na riba isiyobadilika kiwango chake huwa hakibadiliki wakati wote wa kurejesha mkopo
“Kutambua aina za riba kunakuwezesha kupanga kwa usahihi namna ya kurejesha mkopo”, alisema Bw. Kimaro.
Akizungumza baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Wiki ya Utumishi wa Umma, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi, alisema kuwa elimu ya fedha ni muhimu kwa watanzania na akaipongeza Wizara ya Fedha kwa kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa watanzania wote.
Wiki ya Maadhimisho ya Utumishi wa Umma imeanza Juni 16 na inatarajiwa kuhitimishwa Juni 23 mwaka huu ikiwa na kauli mbiu ya “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidigiti ili kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchangia Uwajibikaji”.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi, akisalimiana na Afisa Mkuu wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, baada ya kupata maelezo ya elimu ya elimu ya fedha ambayo ni moja ya huduma inayotolewa katika Banda la Wizara ya Fedha, katika Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi, akiuliza maswali kuhusu masuala ya sekta ya fedha, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma, kulia ni Afisa Mkuu wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro.


Afisa Mkuu wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro akitoa elimu ya usimamizi binafsi wa fedha ili kukuza Uchumi binafsi kwa wakazi wa Dodoma waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Maafisa kutoka Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali, Bw. Eliud Mkiramweni na Bw. Samweli Mkwama, wakitoa elimu ya maandalizi na usimamizi wa bajeti kwa Bw. Mohamed Mkindi, kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Afisa Mkuu wa Kitengo cha Pensheni Wizara ya Fedha, Bi. Joyce Chacky, akitoa elimu ya Pensheni kwa mkazi wa Dodoma, Bw. Frank Lyalumba, alietembelea Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Afisa Mwandamizi wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa, Bw. Sepo Seni, akitoa elimu kuhusu uhimilivu wa deni la Taifa kwa mkazi wa Dodoma, Bw. Dotto Mwatengule, alietembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Afisa kutoka Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali, Bw. Samweli Mkwama, akitoa elimu ya usimamizi wa bajeti kwa Bi. Naumi Kalulu, kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)