Maafisa ugani wapatao 1,701 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za ugani, kupitia mfumo wa kisasa wa M-Kilimo.
Kupitia mfumo huu, Maafisa Kilimo wataweza kuwafikia wakulima wengi kwa wakati mfupi na kuwapa taarifa muhimu kuhusu kanuni bora za kilimo, taarifa za hali ya hewa, masoko ya mazao na mbinu za kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi. Mafunzo haya pia yamewahusisha namna ya kupima udongo na mbinu za uhifadhi wa ardhi katika shughuli za kilimo.
Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Tanzania Food Systems Resilience Program (TFSRP) inayoendeshwa na Wizara ya Kilimo, ambapo yamepangwa kutolewa kwa awamu tatu, ikianza na awamu ya kwanza kuanzia Aprili 14 hadi Juni 20, 2025, ikifuatiwa na awamu ya pili katika mwaka wa fedha 2025/2026, na awamu ya tatu katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Kwa mujibu wa Bi. Paschalina Hayuma, Mratibu kutoka Wizara ya Kilimo, lengo la mpango huu ni kufikia Maafisa Ugani 4,000 na wakulima milioni 3 ifikapo 2026/2027, kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo na kupunguza athari za tabianchi.
Maafisa ugani waliopata mafunzo katika vituo vya MATI Uyole, MATI Igurusi na MATI Inyala, wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa ufanisi mkubwa ili kufanikisha lengo la kuwafikia wakulima zaidi ya milioni 3 kama ilivyopangwa.
Aidha, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuipa Sekta ya Kilimo kipaumbele cha juu, jambo ambalo linaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa Taifa.